Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Serikali ya Marekani yatoa msaada wa magari 34 kusaidia upelelezi wa rushwa

Agosti 1, 2007

Tarehe 1 Agosti, Balozi wa Marekani nchini, Michael L. Retzer, kwa niaba ya Serikali ya Marekani atatoa msaada wa magari 34 aina ya Toyota Rav4 yenye thamani ya zaidi ya dola 400,000 kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili kuongeza uwezo wa taasisi hiyo kufanya upelelezi wa nje. Balozi Retzer, Mkurugenzi wa shirika la misaada la Marekani USAID, Pamela White, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bwana Edward Hoseah watahudhuria sherehe hiyo ya makabidhiano kwenye Ubalozi wa Marekani.

Serikali ya Marekani tayari imetoa mafunzo ya kitaaluma kwa waendesha mashtaka na wapelelezi ili kuimarisha ujuzi wao katika kufanya upelelezi wa kina na shughuli za kipolisi, katika kushughulikia utapeli kwenye ununuzi, na kuongoza mashtaka na kufanya utetezi kortni.

“Uchunguzi wa kina unaoegemea ushahidi imara ni muhimu sana katika kuongoza mashtaka na kufanikisha kuhukumiwa kwa watuhumiwa wa rushwa,” alisema Mkurugenzi Mkuu Hosea. “Magari haya yataimarisha sana uwezo wa TAKUKURU kufanya upelelezi wa nje.”

Msaada huu ni sehemu ya msaada wa dola milioni 11.5 zilizotolewa na Serikali ya Marekani kwa Serikali ya Tanzania, kupitia mfuko wa Millennium Challenge Account Threshold Program, ili kusaidia kujenga uwezo wa nchi kupambana na rushwa. Sehemu ya mpango huo inayohusu utawala wa sheria, inasisitiza uzuiaji, udhibiti, na ukomeshaji wa rushwa katika vyombo muhimu vya sheria.

Mpango huo pia umetoa misaada kwa asasi za kiraia na vyombo vya habari, ili kuboresha uwajibikaji na utawala bora. Mpango wa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari umefanikiwa sana katika kuongeza idadi ya taarifa zinazohusiana na rushwa ambazo huchapishwa na vyombo vya habari kutoka wastani wa 20 kwa mwezi kabla ya kuanzishwa kwa mpango huo, na kufikia 476 mwezi uliopita.