Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Viongozi wawili wa CUF waenda Marekani kuhudhuria mafunzo juu ya serikali za majimbo na serikali za mitaa

Agosti 3, 2005

Naibu Katibu Mkuu wa chama cha CUF, Juma Duni Haji na Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi, Hamad Masoud Hamad wameondoka nchini kuelekea Marekani kushiriki katika ziara ya mafunzo ya mpango wa wageni wa kimataifa, International Visitors programme wa wiki tatu juu ya Serikali za Majimbo na Serikali za Mitaa (State and Local Governments) inayoanza Agosti 4.

Hawa ni wanasiasa ambao wanafahamika sana katika nyanja za kisiasa. Juma Duni Haji amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF tangu 2000. Aliwahi pia kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka 1997 mpaka 2000 na Naibu Mkurugenzi wa Fedha wa chama cha CUF kutoka 1996 mpaka 1997.

Hamad Masoud Hamad amekuwa Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi tangu 2000, na pia Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF tangu 1995. Kuanzia 1995 mpaka 2000 alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na aliwahi pia kuwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu katika chama cha CUF kuanzia 1995 mpaka 1999.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini inasema kwamba, wansiasa hao wawili wataungana na washiriki wengine 23 kutoka nchi mbalimbali katika mafunzo hayo ya wiki tatu yatakayowapeleka Washington DC, Illinois, California, Montana, na New Mexico.

Washiriki wengine wanatoka nchi za Botswana, Cote d'Ivoire, Gaza, Hungary, India, Kenya, Malta, Malaysia, Namibia, Nepal, Nigeria, Philippines, Sierra Leone, Uhispania, Sri Lanka, Uturuki, Uganda, Yemen, Zimbabwe, huku Afrika ya Kusini na Pakistan zikiwakilishwa na washiriki wawili kwa kila nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, lengo la ziara hiyo ni kuelimisha jinsi serikali za mitaa na serikali za majimbo zinavyofanya kazi nchini Marekani, jinsi serikali hizo zinavyohusiana na serikali ya kifederali, na jinsi chaguzi za serikali za mitaa zinavyoandaliwa na kutekelezwa.

Washiriki pia watachunguza utengano wa madaraka kati ya serikali za majimbo na za mitaa, na mgawanyo wa madaraka na majukumu kati ya ngazi hizi mbili za serikali. Pia wataangalia jinsi wananchi binafsi, taasisi za kijamii, na sekta ya biashara zinavyofanya kazi pamoja na serikali za majimbo na za mitaa katika kutoa huduma na kuhakikisha kwamba kuna uwajibikaji..

Wakiwa mjini Washington DC, washiriki wa mafunzo hayo watatembelea Kamati ya Taifa ya Chama cha Republican (Republican National Committee) na Kamati ya Taifa ya Chama cha Democratic (Democratic National Committee) ili kuchunguza muundo wa vyama vya siasa nchini Marekani. Pia watafanya majadiliano kuhusu jinsi ya kuratibu oganaizesheni za kitaifa, kimajimbo na kimtaa, maofisa waliochaguliwa, wagombea na majimbo yao.

Pia watakutana na maofisa waandamizi wa baraza la taifa la utungaji wa sheria katika serikali za majimbo, National Conference of State Legislature (NCSL) kujadili umuhimu wa kushawishi serikali na baraza la Congress kwa niaba ya majimbo. NCSL ni taasisi ambayo haiegemei upande wowote kisiasa inayowahudunia wabunge na wafanyakazi wa majimbo yote 52 kwa kutoa msaada wa kiufundi na kufanya tafiti kuhusu masuala muhimu yanayokabili majimbo.

Huko Illinois, washiriki wataangalia mfano wa msingi kuhusu mfumo wa utawala nchini Marekani, ambako halmashauri ya mji inabeba mamlaka ya kisiasa. Aidha, watakutana na vyombo vya dola vya wilaya kujifunza juu ya hatua za kulinda sheria katika ngazi hiyo, pamoja na uhusiano kati ya polisi na jamii.

Wakiwa California, washiriki wataelimishwa kuhusu mafunzo yanayotolewa kwa wabunge wapya na wafanyakazi wapya wa Bunge. Pia watakutana na maafisa wa Gavana Arnold Schwarzenegger wanaoshughulikia kutekeleza mabadiliko ya mbinu za usimamizi yanayolenga kupunguza deni la serikali ya jimbo. Watafanya pia majadiliano kuhusu majukumu ya Gavana na uhusiano wake na serikali za mitaa na serikali ya kifederali.

Huko Montana, washiriki hao watajifunza kuhusu fursa ya mafunzo na huduma wanazopata maafisa wa serikali za mitaa kwenye kituo cha serikali za mitaa huko Bozeman, ambacho hufanya kazi pamoja na maafisa wa jiji, wilaya, na jimbo ili kuboresha utendaji kazi na uwajibikaji serikalini.

Katika kituo chao cha mwisho huko New Mexico, washiriki watatembelea gazeti kubwa la kila siku la Santa Fe na kujifunza jinsi vyombo vya habari vinavyofanya kazi ya kusimamia uwazi na uwajibikaji.

- Translation -
This content is also available in English