Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Serikali ya Marekani kutoa zaidi ya dola 800,000 kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya UKIMWI Tanzania

Agosti 3, 2005


Iringa - Kupitia msaada unaotolewa na mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR), zaidi ya dola 800,000 zitatolewa ili kuimarisha mipango ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI inayowalenga vijana, katika hafla ya kutoa tuzo itakayofanyika katika Bustani za Manispaa ya Iringa siku ya Ijumaa, Agosti 5, 2005.

Asasi nne zisizo za kiserikali zinazofanya kazi katika mikoa ya Dar es Salaam na Iringa zitapata tuzo hiyo kupitia mpango wa misaada ya ushindani (Competitive Grants Program). Mashirika hayo ni: mtandao wa kupinga ukeketaji AFNET (Anti-Female Genital Mutilation Network), chama cha kuendeleza watoto yatima COCODA (Community Concerns of Orphans and Development Association), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), na chama cha kuendeleza Wilaya ya Makete, SUMASESU (Support Makete to Self Support).

Misaada hii itaongeza juhudi za kuleta mwamko, ufahamu na stadi za maisha juu ya janga la UKIMWI; itajenga uwezo wa maeneo husika na kuwawezesha vijana, wazazi, jamii na viongozi wa kidini katika jitihada za kuzuia maambukizi ya UKIMWI.

Mkurugenzi Mkazi wa shirika la misaada la Marekani (USAID) nchini Tanzania, Pamela White na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Mheshimiwa William Lukuvi watakabidhi hundi katika hafla ya kutoa tuzo hizo.

Mpango wa misaada ya ushindani (Competitive Grants Program) ni sehemu ya shughuli za mtandao wa vijana Tanzania, YouthNet/Tanzania. Huu ni mpango wa miaka mitano unaoratibiwa na kusimamiwa na shirika la kimataifa linaloshughulikia afya ya familia, Family Health International (FHI). Mpango huu ulibuniwa ili kusaidia miradi mikubwa katika juhudi za kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa vijana wa mikoa ya Dar es Salaam na Iringa.

Mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR), kupitia Vituo vya Kudhibiti Magonjwa vya Marekani (Centers for Disease Control), Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Huduma ya Kujitolea ya Peace Corps, na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), unasaidia juhudi za Tanzania katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI. Kupitia mpango huu wa PEPFAR, serikali ya Marekani inasaidia juhudi za kitaifa za kuzuia, kutibu na kuwatunza waathirika nchini kote Tanzania.

Maelezo yafuatayo yanahusu miradi ya asasi nne zilizoshinda tuzo:

AFNET (Anti-Female Genital Mutilation Network).
Mtandao wa AFNET unahamasisha kuacha ngono kabisa na kuwa mwaminifu kwa mpenzi mmoja aliyepima, na kupunguza tabia hatari ya kufanya ngono zembe miongoni mwa vijana katika wilaya za Iringa na Kilolo, mkoani Iringa. AFNET itawajengea vijana 25,000 stadi za maisha katika kata 12 za wilaya ya Iringa na Kilolo ili waweze kuacha ngono kabisa au kuwa waaminifu. AFNET pia itaendesha mafunzo kwa wazazi juu ya mbinu za kuzuia maambukizi ya UKIMWI na stadi za mahusiano katika afya ya uzazi kwa vijana, pamoja na kuongeza idadi ya vijana wanaopata ushauri nasaha na kupima UKIMWI.

COCODA (Community Concerns of Orphans and Development Association). Chama cha COCODA kinalenga katika kupunguza hatari ya maambukizi ya UKIMWI miongoni mwa vijana wenye umri kuanzia miaka 10 mpaka 24 katika wilaya za Njombe na Ludewa, mkoani Iringa. COCODA itahamasisha mwamko juu ya hatari zinazowakabili vijana kuhusiana na ngono na afya ya uzazi, wao wakiwa miongoni mwa wadau wakubwa na walengwa katika ngazi ya wilaya na jumuiya; kujenga uwezo mpana wa kusaidia kuzuia tabia za hatari katika umri wa vijana uliotajwa na kutoa taarifa sahihi kwa vijana wa umri huo kupitia utoaji wa elimu kwa rika hilo juu ya namna ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI na kuboresha afya ya uzazi miongoni mwao.

BAKWATA (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania). BAKWATA inalenga kuwajengea uwezo viongozi wa Kiislamu, walimu na wazazi katika kuzuia maambukizi ya UKIMWI miongoni mwa vijana katika mikoa ya Dar es Salaam na Iringa. BAKWATA itaongeza mwamko miongoni mwa viongozi wa Kiislamu katika kuzuia maambukizi ya UKIMWI na afya ya uzazi kwa vijana, itaongeza ufahamu, stadi za maisha kwa walimu (kwenye madrasa, shule za msingi na sekondari) katika mikoa ya Iringa na Dar es Salaam, na kuhamasisha wazazi juu ya umuhimu wa uzuiaji wa maambukizi ya UKIMWI na uelewa wa afya ya uzazi na maadili kwa watoto wao.

SUMASESU (Support Makete to Self Support). Chama cha SUMASESU kinalenga katika kupunguza uwezekano wa vijana wa miaka kati ya 10 na 24 kuambukizwa na UKIMWI na matatizo mengine yahusianayo na afya ya uzazi. SUMASESU itaboresha uwezo wa jamii katika wilaya ya Makete, mkoani Iringa, kuchukua hatua katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI miongoni mwa vijana, kuboresha maelewano katika masuala ya UKIMWI na afya ya uzazi miongoni mwa vijana, na kuwapa vijana mbinu na maarifa ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya UKIMWI na matatizo yahusianayo na afya ya uzazi.

Tuzo ndogo nne, zilizochaguliwa na mfuko wa misaada ya haraka, Rapid Response Grants wa FHI-YouthNet, pia zitatolewa katika hafla hiyo.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Mr. Daudi Nasib
YouthNet/Tanzania
Family Health International
Ofisi: 260-1866/7
Selula: 0744-222 377

- Translation -
This content is also available in English