Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Ubalozi wa Marekani waadhimisha miaka tisa tangu kulipuliwa

Agosti 7, 2007

Leo (Agosti 7), wafanyakazi wa Ubalozi wa Marekani jijini Dar-es-Salaam waliadhimisha mwaka wa tisa tangu kulipuliwa kwa Balozi za Marekani Afrika Mashariki. Baada ya hotuba fupi iliyotolewa na Balozi wa Marekani nchini, wafanyakazi wote wa Ubalozi walisimama kimya kwa muda wa dakika moja ilipofika saa 4:39 asubuhi.

Kama kumbusho dhahiri kwamba ugaidi hauna tabia ya kubagua, wote waliouawa kwenye mashambulizi hayo jijini Dar-es-Salaam walikuwa Watanzania. Kwa kuwakumbuka wote waliokufa kwenye mashambulizi ya balozi hizo, Balozi Michael Retzer, akifuatana na Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania, Bwana Robert V. Royall, aliweka shada la maua karibu na kumbukumbu ya “Tunakumbuka Agosti 7” ya milango ya asili ya Zanzibar iliyo ndani ya Ubalozi.

Balozi Retzer alisema, “miaka tisa iliyopita, magaidi walijaribu kuharibu uhusiano wa amani ambao Marekani inaufurahia na nchi za Afrika ya Mashariki. Lengo la magaidi hawa lilikuwa ni kuweka ufa kwenye uhusiano wetu, ili waweze kuendeleza fujo na vurugu. Mpango wao wa kutisha haukuweza kufanikiwa. Pamoja na kwamba tulipoteza marafiki na wafanyakazi wenzetu asubuhi hiyo ya majonzi, lakini tuliweza kujenga mshikamano na uaminifu kati yetu wenyewe na nchi zetu.”

Ifuatayo ni hotuba fupi ya Balozi Retzer:

Maadhimisho ya miaka tisa tangu mashambulizi ya Agosti 7, 1998 kwenye Balozi za Marekani katika miji ya Dar-es-Salaam na Nairobi

Huu ni wakati wa majonzi makubwa, lakini ninashukuru kwamba tuna fursa ya kukusanyika pamoja na kuwakumbuka wafanyakazi wenzetu na marafiki zetu waliopoteza maisha yao kupitia vitendo hivi vya kikatili vya ugaidi. Siku hii miaka tisa iliyopita, milipuko ilisikika jijini hapa na kwa majirani zetu kaskazini, na kusababisha moto na vifusi, huku hofu kubwa ikizikumba Balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania. Wengi wenu mlikuwa hapa kwenye Ubalozi wa Marekani wakati wa mlipuko huo. Ninaweza tu kuhisi hofu na wasiwasi mlioupata wakati huo.

Jijini Dar-es-Salaam, watu 10 walipoteza maisha yao, na zaidi ya 85 walijeruhiwa. Tulikuwa na bahati kwa maana ya kwamba, umwagaji damu haukuwa mkubwa kama jijini Nairobi ambako watu 213 waliuawa na zaidi ya 4,000 kujeruhiwa. Wale walioangamia kwenye milipuko hiyo daima watabaki katika mioyo, maombi, na fikra zetu.

Alimradi magaidi bado wanaendelea kuwadhuru raia wasio na hatia ulimwenguni kote, Marekani itasimama imara kufuatilia uhuru katika nchi zinazozalisha ugaidi. Ni lengo letu kuhakikisha amani ulimwenguni kote. Vita dhidi ya ugaidi inazidi kufanikiwa. Kuungwa mkono kwa Marekani na nchi marafiki, zikiwemo Tanzania na Kenya, kumesaidia kuhakikisha kwamba hakuna gaidi atakayefanikiwa kujenga hofu na wasiwasi miongoni mwa raia ulimwenguni kote.

Miaka tisa iliyopita, magaidi walijaribu kuharibu uhusiano wa amani ambao Marekani inaufurahia na nchi za Afrika ya Mashariki. Lengo la magaidi hawa lilikuwa ni kuweka ufa kwenye uhusiano wetu, ili waweze kuendeleza fujo na vurugu. Mpango wao wa kutisha haukuweza kufanikiwa.

Pamoja na kwamba tulipoteza marafiki na wafanyakazi wenzetu asubuhi hiyo ya majonzi, lakini tuliweza kujenga mshikamano na uaminifu kati yetu wenyewe na nchi zetu.” Ninaona fahari kuhusu urafiki tulioujenga na Tanzania tangu wakati huo, na pia tunaona fahari kwamba tumeweza kuimarisha uhusiano wetu.

Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, Waziri wa zamani wa Marekani wa Mambo ya Nje, Madeleine Albright, aliungana nasi kwenye jiwe la kumbukumbu lililo karibu na lango la Ubalozi wetu. Albright aliwahi kusema kwamba, wale waliokufa kwenye mashambulizi hayo ya mabomu walikuwa watendaji wa kazi ya Marekani: kuimarisha maendeleo, kujenga amani, kuunga mkono haki, kupambana na magonjwa. Kazi yetu inaendelea hadi leo.

Nilidhani ni jambo jema kwamba leo tuweke shada la maua karibu na milango mikubwa yenye asili ya Zanzibar iliyo juu ya ngazi hizi. Kumbukumbu ya “Tunakumbuka Agosti 7” iliyochongwa na Munir Salim Omar, imekuwa ni kumbusho kubwa kwangu kila siku, juu ya hasara ambayo mataifa yetu mawili yaliipata miaka tisa iliyopita.

Mara nyingi huwa ninawaonyesha wageni wetu mashuhuri milango hii na kusema kwamba, Watanzania walikuwa wahanga wa kwanza wa kikundi cha Al-Qaeda. Umbo kubwa la milango hii linaleta hisia za nguvu na usalama kwa wafanyakazi wetu, kwa nchi zetu mbili, na pia kwa ulimwengu. Pamoja, tutalishinda tishio la ugaidi, na ninaamini kwa dhati kwamba, Tanzania na Marekani kamwe hazitapatwa tena na msiba wa kutisha kama ule wa Agosti 7, 1998.

Ni kwa unyenyekevu, heshima, na taadhima kubwa tumekusanyika kuwaenzi waliopoteza maisha yao:

Yusuf Shamte Ndange
Saidi Nankungu Rogath
Ramadhani H. Mahundi
Mtendeje Rajabu Mbegu
Abdallah Mohamed Mnyolya
Abbas William Mwila
Bakari Yusuf Nyumbu
Elia Elisha Paul
Dotto Lukua Ramadhani
Abdulrahaman Abdullah