| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Wahudumu wapya 36 wa Huduma ya Kujitolea ya Peace Corps waapishwa Kilosa
August 16, 2006
Jumatano Agosti 16, 2006, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Retzer aliapisha kikundi cha wahudumu wapya 39 wa Huduma ya Kujitolea ya Peace Corps katika Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro. Wahudumu hao watafanya kazi kwa muda wa miaka miwili katika vijiji 39 kwenye mikoa 15 Tanzania Bara na mikoa 5 Visiwani Zanzibar.
Balozi Retzer alisema kwamba wahudumu hao watafanya kazi kwenye jamii walizopangiwa katika sekta muhimu za mazingira na afya. “Takriban nusu yao watakuwa wakifanya kazi katika miradi ya kutunza mazingira, na waliobaki watajishughulisha na masuala ya elimu ya afya, hususan uhamasishaji kuhusu UKIMWI na mbinu za kujikinga nao,” alisema.
Alisema kwamba wahudumu watakaofanya kazi kwenye miradi ya kutunza mazingira watatumia mbinu zitakazoboresha kipato cha wananchi ili kufanikisha usimamizi bora wa mazingira. Mbinu hizi zinawaonyesha wananchi jinsi ya kujiongezea kipato chao kwa kufanya mabadiliko madogo tu katika mfumo wa maisha yao, au jinsi ya kufanya biashara.
Balozi Retzer alisema kwamba wahudumu watakaojishughulisha na miradi ya afya watashirikiana na walimu, wanafunzi, pamoja na vijana walioacha shule ili kuhakikisha kuwa taarifa zinazohusu UKIMWI zinawafikia walengwa walioathirika.
Sherehe ya kuapishwa ambayo ilifanyika Wilayani Kilosa ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Bwana Wilson Mkama, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Meja Jenerali mstaafu Saidi Kalembo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Athuman Mdoe, pamoja na familia za wananchi waliojitolea kuwa wenyeji wa wahudumu hao wakati wa mafunzo yao.
Balozi Retzer aliwaambia wahudumu hao na wageni waalikwa kwamba, Huduma ya Kujitolea ya Peace Corps imekuwa ikifanya kazi nchini Tanzania kwa muda wa miaka 34 sasa, na kwamba uhusiano kati ya Marekani na Tanzania unazidi kuimarika, na misingi yake ni kuheshimiana baina ya pande zote mbili. “Baada ya kumalizika kwa Vita Baridi, na kwa kuwa sote tuna malengo ya pamoja, kwa mfano katika harakati za kuleta maendeleo ya kiuchumi, kuboresha elimu, pamoja na kupiga vita umaskini, uhusiano kati ya nchi zetu mbili umeendelea kuimarika. Mashambulizi ya kutisha ya 1998 dhidi ya Ubalozi wa Marekani hapa nchini yameimarisha azma ya nchi zetu mbili kuwa macho dhidi ya tishio la ugaidi,” aliongezea Balozi Retzer.
Alisema kwamba, hivi sasa Marekani na Tanzania zinashirikiana kwa karibu katika masuala haya ya kupambana na ugaidi, vita dhidi ya UKIMWI na malaria, kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo, pamoja na kuimarisha mifumo na michakato ya demokrasia.
Balozi Retzer alisema, “Ninaona fahari kwamba Marekani imekuwa ikiongoza vita dhidi ya UKIMWI ulimwenguni kwa kutoa mabilioni ya dola kufadhili shughuli za tiba, kinga na huduma za kuwatunza waathirika, huku tukishirikiana kwa karibu na wadau katika nchi zaidi ya 100 ulimwenguni kote.
Tanzania ni moja ya nchi 15 duniani zilizopewa kipaumbele kuhusu msaada maalum wa kupambana na UKIMWI – mpango wa dola bilioni 15 kwa muda wa miaka 5 – kwa sababu nchi hizi zinawakilisha takriban nusu ya maambukizi ulimwenguni kote.



