Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Wahudumu wapya wa kujitolea wa Huduma ya Peace Corps waanza kazi katika vituo mbalimbali nchini kote

Agosti 17, 2005


Jumatano Agosti 17, 2005, Kaimu Balozi wa Marekani D. Purnell Delly alikiapisha kikundi cha wahudumu wapya wa kujitolea wa Huduma ya Peace Corps kwenye hafla iliyofanyika kwenye Chuo cha Kilimo cha Ilonga wilayani Kilosa, katika mkoa wa Morogoro. Kikundi hiki cha wahudunu kitafanya kazi kwa muda wa miaka miwili katika vijiji mbalimbali nchini kote Tanzania, wakielekeza juhudi zao hususan katika usimamizi endelevu wa mazingira na kutoa elimu ya afya bora. Wilaya watakamofanya kazi ni pamoja na Mwanga, Mufindi, Njombe, Singida, Hanang, Newala, Karatu na Morogoro.

Wahudumu hawa 32 wanaifanya idadi ya wahudumu wote wanaofanya kazi nchini Tanzania kufikia 133. Zaidi ya nusu ya wahudumu wapya watafanya kazi ya kutoa elimu ya afya, kwa lengo la kuwaelimisha vijana kuhusu janga la UKIMWI na kuwasaidia kupata stadi zinazohitajika kujenga tabia za kuzingatia afya bora.

Katika hotuba yake, Kaimu Balozi alisistiza kuhusu azma ya serikali ya Marekani kutoa dola bilioni 15 kusaidia mapambano dhidi ya janga la UKIMWI duniani kote. Huduma ya kujitolea ya Peace Corps ni mojawapo ya taasisi zinazotekeleza mpango huu ambao unaitwa mpango wa dharura wa Rais wa kupunguza makali ya UKIMWI, (PEPFAR). Kaimu Balozi alisema kwamba katika mpango huo wa PEPFAR, "kuongeza uelewa miongoni mwa vijana kuhusu janga la UKIMWI ni uwekezaji bora kabisa katika mustakabali wao." Aliwapongeza wahudumu wa Peace Corps kwa kujitolea kufanya kazi hii muhimu na aliwahimiza wote kuongea waziwazi na vijana kuhusu janga la UKIMWI kila wanapopata nafasi.

Wahudumu wengine wa huduma ya Peace Corps watakuwa wakifanya kazi hususan katika miradi inayohusiana na utunzaji wa mazingira, wakitumia mbinu zitakazohakikisha kwamba kipato cha wadau kinaongezeka, ili kufanikisha usimamizi bora wa mazingira. Mbinu hizi ambazo zinatumika sana nchini Marekani na penginepo, zinaruhusu wananchi kuongeza kipato chao kwa kufanya mabadiliko madogo katika maisha yao. Mfano mzuri ni matumizi ya majiko yanayotumia nishati ndogo ambayo huchangia kupunguza gharama za maisha kwa familia na wakati huo huo kufanikisha matumizi bora ya maliasili.

Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Maimuna Tarishi, atakuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo ambayo pia itahudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Issa Machibya, viongozi wa kijiji, pamoja na wananchi waliokuwa wenyeji wa wahudumu hao wa kujitolea wakati wa mafunzo yao ya nje ya wiki tisa.

Huduma ya Peace Corps ambayo ilianzishwa 1961 na Rais John F. Kennedy, ni taasisi ya serikali ya Marekani ambayo inawahudumia wafanyakazi wa kujitolea 7,300 katika nchi takriban 70 duniani kote. Tanzania ilikuwa ni moja ya nchi za kwanza kabisa kupokea wahudumu wa Peace Corps 1962. Huduma hiyo inajivunia kuweza kutoa mchango wake katika shughuli za kiufundi na kiutamaduni bila kufungamana na upande wowote wa siasa au madhehebu. Lengo lake ni kutumia rasilimali zinazopatikana katika jamii kuwasaidia wananchi waweze kujisaidia wenyewe. Huduma ya Peace Corps inafanya juhudi kuimarisha amani na urafiki ulimwenguni kote kwa kutimiza malengo matatu ya msingi: 1) kutoa huduma ya wafanyakazi wa kujitolea wanaochangia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi zinazowakaribisha; 2) kujenga uelewa mzuri kuhusu Wamarekani miongoni mwa wananchi wanaohudumiwa na wafanyakazi wa Peace Corps; na 3) kuboresha uelewa wa Wamarekani juu ya ulimwengu na watu wake.

- Translation -
This content is also available in English