Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Press Releases > Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Tanga- Horohoro waingia hatua mpya
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Tanga- Horohoro waingia hatua mpya

26 Agosti 2009

Siku ya Alhamisi, tarehe 20 Agosti, Maafisa wa Mfuko wa Changamoto za Milenia – Tanzania (MCA-T) na wale wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), pamoja na viongozi wa Mkoa, waliendesha mkutano wa wazi mjini Tanga ambapo walikutana na makampuni mbalimbali yanayoshindana kupata zabuni ya ukarabati na ujenzi wa barabara kutoka Tanga hadi Horohoro. Baada ya mkutano huo, watendaji wa MCA-T na TANROADS pamoja na waombaji wa zabuni walitembelea eneo la mradi ambalo ni kilomita zote 68 za barabara hiyo. Kwa Mujibu wa Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), Bw. Karl Fickenscher, “tukio hili linaashiria hatua nyingine muhimu katika utekelezaji wa mradi wa barabara ya Tanga hadi Horohoro.” Kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uwazi katika taratibu za manunuzi na utoaji zabuni wenye ushindani wa miradi mikubwa ya ujenzi wa miundo mbinu, MCC na MCA-T hutumia utaratibu wa manunuzi na utoaji zabuni wenye awamu kadhaa (multi-phase procurement process). Katika awamu ya kwanza, makampuni kutoka duniani kote hualikwa ili kuelezea uzoefu, utaalamu na rasilimali walizonazo zitakazowawezesha kukamilisha mradi unaokusudiwa wakibainisha pia muda na bajeti. Jambo hili hufanyika kwa kutoa matangazo mengi ndani na nje ya Tanzania. Hakuna masharti kwamba ni lazima mradi ununue vifaa kutoka Marekani, au masharti yoyote yanayofungamanishwa na fedha zinazotolewa na MCC katika utaratibu wake wa manunuzi. Ni makampuni yale tu yanayofanikiwa kuvuka katika hatua hii ya awali ndiyo yanayoruhusiwa kuendelea katika duru ya pili ya maombi ya zabuni. Kwa mujibu wa Bw. Fickenscher, “kwa kubuni utaratibu huu wa kishindani, MCC na MCA-T wanalenga katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na ushindani mkubwa miongoni mwa makampuni yale tu yenye sifa nzuri zinazotakiwa katika mradi husika, hivyo kuongeza uwezekano wa mradi kutekelezwa kwa kasi, ubora na mafanikio yaliyokusudiwa.” Makampuni yote yaliyoshiriki katika mkutano wa zabuni huko Tanga yalikuwa yanevuka katika hatua ya awali na hivyo kutakiwa kuwasilisha maombi yao ya mwisho ya zabuni, maombi ambayo mwisho wa kupokewa kwake ni mwezi Septemba.

Barabara ya Tanga – Horohoro ni mojawapo katika ya barabara kuu kadhaa zitakazojengwa au kufanyiwa ukarabati mkubwa chini ya Mradi wa “Barabara Kuu za Tanzania Bara” unaotekeleza kama sehemu ya Mkataba wa Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Compact) uliosainiwa na Rais aliyepita wa Marekani George Bush na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2008. Barabara nyingine zitakazojengwa sambamba na ile ya Tanga-Horohoro ni ile ya kilomita 224, kutoka Tunduma kupitia Laela hadi Sumbawanga na ile ya kilomita 139 kutoka njia panda ya Peramiho hadi Mbinga, na baadaye mashariki hadi Nantumbo. Kwa kupitia mkataba wa MCC, watu wa Marekani wanafadhili pia miradi mingine kadhaa ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo ukarabati wa barabara za maeneo ya vijijini kisiwani Pemba zenye urefu wa kilomita 36, uboreshaji wa uwanja wa ndege kisiwani Mafia na kutoa msaada wa kitaalamu kwa Wakala wa Barabara - TANROADS ili kuimarisha uwezo wao wa kusimamia, kutunza na kufanyia marekebisho barabara za Tanzania. Mkataba huu unajumuisha pia kusaidia miradi ya miundombinu katika sekta za nishati na maji. Jumla ya Dola za Kimarekani 698.1 milioni zitatolewa chini ya mkataba huu katika kipindi cha miaka mitano (2008-2013).