| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Miradi 15 yapokea Sh. Milioni 87.9 kutoka kwenye mfuko maalum wa Balozi wa Marekani wa kusaidia maendeleo katika jamii
Agosti 30, 2006
Jumatano Agosti 30, 2006 Balozi wa Marekani nchini Michael L. Retzer alitia saini mikataba 15 na asasi za kijamii ambazo zitapata kiasi cha Sh. 87, 900,000 kutoka kwenye mfuko maalum wa Balozi wa kusaidia maendeleo katika jamii, Ambassador’s Special Self-Help Fund (ASSHF) wakati wa sherehe iliyofanyika kwenye Ubalozi wa Marekani jijini Dar-es-Salaam. Hii inafanya jumla ya misaada iliyotolewa na mfuko huo tangu 2001 kufikia Sh. milioni 617.7.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ubalozi wa Marekani, mfuko huo wa Balozi unaoshughulikia maombi ya misaada kwa miradi midogomidogo ya kijamii ulianzishwa 1965 na umefanikiwa kuboresha hali ya maisha na uchumi katika ngazi za vijiji kuanzia Arusha mpaka Zanzibar. Misaada ya mfuko wa ASSHF imesaidia kuboresha hali ya usafi, elimu, maendeleo ya kiuchumi na sekta ya kilimo.
Kwenye sherehe hiyo ya kutia saini mikataba ya miradi itakayofadhiliwa na mfuko wa ASSHF, Balozi Retzer alitoa hundi kwa wawakilishi wa vikundi kutoka: Kituo cha Mahango cha kutoa elimu kwa watoto yatima, Mbeya; Kituo cha kuhudumia walimu na jamii, Masasi, Mkoa wa Mtwara; Kituo cha kuleta maendeleo ya kiuchumi na kutunza mazingira Arusha; Umoja wa Kinamama Kusaidiana Kigamboni, Dar-es-Salaam; Taasisi ya kutoa huduma za kuwasaidia wananchi Karagwe – Mavuno Improvement for Community Relief and Services, Mkoa wa Kagera; Chama cha Walemavu katika Mikoa ya Tabora na Mbeya; Wakulima Bushumba, Muleba, Mkoa wa Kagera; na Kituo cha Bethlehem, Ifakara, Mkoa wa Morogoro.
Miradi mingine ni Paroko ya Mt. Teresa Kasanga, Mkoa wa Morogoro; kampuni ya kusindika chakula ya Feceh Food Processing Enterprise, Moshi; Mfuko wa Maendeleo Wawi, Pemba; chama cha kuendeleza wananchi cha Human Development Strategies Association, Kimamba, Mkoa wa Morogoro; Chama cha Christian Association for Development and AID, Musoma; pamoja na Shule ya Matemwe, Zanzibar.
Watunukiwa wa mwaka huu walichaguliwa kutoka kwenye kundi la taasisi 150 zilizoingia kwenye uchaguzi wa mwisho, na wote wamethibitisha wana moyo wa kujitolea.
Balozi Retzer alisema: “Katika kila mradi, jamii husika imetoa mchango mkubwa kabla ya kuomba msaada kwetu. Katika baadhi ya miradi, wananchi wamechanga pesa. Wengine wametoa mfuko mmoja au miwili ya sementi. Karibu katika miradi yote, wananchi wamekubali kuchangia nguvu yao. Lakini katika miradi yote, kila jamii ilitafuta msaada kwanza ndani yake, kabla ya kuangalia nje.”
Mfuko wa ASSHF umekipa Kituo cha Kijiji cha Mahango cha kutoa elimu kwa watoto yatima Sh. 2,520,000 ambazo zitawasaidia zaidi ya watoto yatima 80 wanaohitaji makazi, matunzo, pamoja na elimu. Wananchi wa Mahango wametoa kiwanja cha kujengea nyumba ya kulala watoto na kituo cha elimu. Huko Masasi, mfuko umetoa Sh. 3,762,360 kujengea tenki la kuhifadhi maji litakalotumiwa na wananchi 20 wa kijiji cha Nyasa. Huko Arusha, mradi wa kuleta maendeleo ya kiuchumi na kutunza mazingira, Community Action for Development, Economic and Environment Conservation Trust umepewa Sh. 7,100,100 zitakazotumika kuzalisha miche ya miti ya matunda ambayo itasambazwa kwa vijana na wanawake katika wilaya za Monduli, Arumeru na Arusha.
Kikundi cha UKIKU Kigamboni kimepokea Sh. 4,529,700 kusaidia mradi wa kutengeneza matofali; Taasisi ya kutoa huduma za kuwasaidia wananchi Karagwe – Mavuno Improvement for Community Relief and Services, ilipokea Sh. 7,383,600 kusaidia ujenzi wa matenki ya maji. CHAWATA, tawi la Tabora imepokea Sh. 7,497,000 zitakazotumika kutengenezea baiskeli za walemavu na pia kutengenezea milango na fremu za madirisha. Kikundi cha Wakulima Bushumba, Bukoba kimepokea Sh. 5,670,000 kuboresha uzalishaji na kiwango cha ubora wa kahawa ya organic ili iweze kupata bei nzuri zaidi kwenye soko.
Kituo cha Bethlehem cha Ifakara ambacho kinahudumia na kutoa mafunzo kwa watoto wenye ulemavu wa akili kimepokea Sh. 7,131,600 za kujengea mtambo wa kuzalisha nishati ya jua (solar) kwenye nyumba za kulala, ili kupunguza gharama za umeme. Paroko ya Mt. Teresa huko Kasanga, Morogoro ilipewa Sh. 3,477,600 za kununulia mashine ya kusaga ili kuwasaidia wanawake na watoto ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda kusaga mahindi yao. Kijiji hiki kiko umbali wa km 144 kutoka mjini Morogoro, kwenye milima ya Uluguru.
Mradi mwingine huko Moshi ni ule wa Feceh Food Processing Enterprise ambao umepokea Sh. 7,560,000 kusaidia usindikaji wa matunda na mbogamboga. Kikundi hiki cha watu 32 kinazalisha achari ya maembe, pilipili, siagi ya karanga, maembe na kisamvu kilichokaushwa. Mradi wa CHAWATA, tawi la Mbeya umepokea Sh. 4,410,000 za kununulia mashine ya kukamua mafuta, wakati mfuko wa maendeleo wa Pemba Development Trust Fund umepata Sh. 8,820,000 ili kumalizia ujenzi wa madarasa matatu na kuyawekea vifaa.
Miradi mingine ni Human Development Strategies Association, Kimamba, Morogoro ambao umepata Sh. 2,520,000 za kuimarisha huduma ya maji kwa wanakijiji 14,506. Taasisi ya Christian Association for Development and Aid ya Musoma imepokea Sh. 7,912,800 za kununulia vifaa vya maabara ya zahanati. Shule ya Matemwe, Zanzibar, imepokea Sh. 7,660,800 za kununulia madawati. Ni asilimia 30 tu ya wanafunzi kwenye shule hiyo wana madawati.



