Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Ubalozi wa Marekani waadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa sita tangu mashambulizi ya Septemba 11
Septemba 11, 2007
Septemba 11, wafanyakazi wa Ubalozi wa Marekani jijini Dar-es-Salaam waliadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa sita tangu mashambulizi ya September 11, 2001 nchini Marekani. Wafanyakazi wote walikusanyika karibu na mlingoti, chini ya bendera ya Marekani iliyokuwa ikipepea nusu mlingoti na kusimama kimya kwa muda ilipofika saa 9.46 mchana (muda ambao ndege ya kwanza ilipogonga Mnara wa Kaskazini wa jengo la Kituo cha Kimataifa cha Biashara - World Trade Centre: Saa 2.46 asubuhi huko New York.)
Mmoja wa wafanyakazi wa Ubalozi alisema, “Kumbukumbu ya sita ya mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani inatupa fursa ya kudhihirisha msimamo wetu wa kulaani vitendo vyote vya kigaidi. Wote tuungane pamoja kuweka upya juhudi zetu za dhati kujenga dunia yenye amani ili vitendo kama hivyo visiweze kutokea tena.”
Katika kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka huu, Rais George W. Bush alitangaza kwamba, “Siku ya Septemba 11, 2001, ilikuwa ni siku iliyoleta mabadiliko makubwa katika historia ya Marekani. Siku hiyo ya kutisha, taifa letu liliona sura ya uovu, wakati wanaume 19 walipotushambulia kwa ukatili na kuua bila sababu watu wa rangi, mataifa na dini mbalimbali. Wakati huu wa Siku ya Uzalendo (Patriot Day), tunawakumbuka wahanga ambao hawakuwa na hatia yoyote, na tunawaenzi wafanyakazi jasiri wa idara za kuzima moto, polisi, huduma za dharura, pamoja na wananchi wa kawaida waliohatarisha maisha yao ili wengine waweze kuishi.”
“Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, Marekani iliamua kwamba tutachukua hatua kali dhidi ya maadui wetu, na kwamba hatutatofautisha baina ya magaidi na wale wanaowapa hifadhi au kuwaunga mkono. Wamarekani wote wanawaheshimu wanaume na wanawake wa majeshi yetu waliojitoa mhanga, wafanyakazi wetu hodari wa vyombo vya usalama wa raia, sheria, na usalama wa taifa, pamoja na maelfu ya watu wengine wanaofanya kazi kwa bidii kila siku, kuilinda nchi yetu, kulinda uhuru wetu, na kuzuia mashambulizi mengine yasitokee,” alisema Rais Bush.
Rais alisema kwamba, moyo wa wananchi wa Marekani ndiyo chimbuko la nguvu za Marekani, na miaka sita iliyopita, Wamarekani walijitokeza kuwasaidia majirani zao waliohitaji msaada. “Wakati huu wa Siku ya Uzalendo, tunawaombea wale waliofariki, pamoja na familia zao. Tunajitolea kuwasaidia wengine na kudhihirisha moyo wa huruma wa wananchi wetu. Wakati huu wa huzuni, tunajitolea upya kujenga msingi wa amani, tukiwa na imani katika malengo yetu, pamoja na maisha yetu huru.”




