Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Mfuko maalum wa Balozi wa Marekani wa kusaidia maendeleo katika jamii watoa Sh. milioni 80 kusaidia miradi 12

Septemba 13, 2005


Jumanne Septemba 13, 2005 Balozi wa Marekani nchini Michael L. Retzer alitia saini mikataba 12 na asasi za kijamii ambazo zitapata kiasi cha Sh. 79,590,067.00 kutoka kwenye mfuko maalum wa Balozi wa kusaidia maendeleo katika jamii, Ambassador's Special Self-Help Fund (ASSHF) kwenye sherehe iliyofanyika kwenye Ubalozi wa Marekani jijini Dar-es-Salaam. Hii inafanya jumla ya misaada iliyotolewa na mfuko huo tangu 2001 kufikia Tsh. milioni 528.

Kwa mujibu wa msemaji wa Ubalozi wa Marekani John Haynes, mfuko huo wa Balozi una historia ndefu ya ushirikiano na wananchi wa Tanzania. Mpango huu wa kipekee ulioanzishwa 1965 una lengo la kuboresha hali ya maisha na uchumi katika ngazi za vijiji. Kuanzia Arusha mpaka Zanzibar, misaada ya mfuko wa ASSHF imewahi kusaidia kuboresha usafi, elimu, maendeleo ya kiuchumi na kilimo. Mfuko wa ASSHF unadhihirisha kujitoa kwa dhati kwa Ubalozi wa Marekani kuleta maendeleo katika jamii na kujenga urafiki na wananchi wa Tanzania.

Lengo la mfuko wa Balozi ni kuimarisha ari ya kujitegemea kwa kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kujikwamua; kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo inanufaisha jamii nzima. "Michango ya jamii kupitia kazi ya kujitolea, usimamizi na nyenzo ni muhimu katika kufanikisha miradi inayofadhiliwa na mfuko wa ASSHF," alisema Haynes.

Watunukiwa wa mwaka huu wataitumia misaada hiyo kwa shughuli mbalimbali, zikiwemo za ujenzi wa bweni la wasichana; ununuzi wa miche ya miti na nyenzo za kuendesha bustani; kuanzishwa kwa huduma ya kivuko kwa wakazi wa kisiwa kimoja; na uimarishaji wa ushirika wa wakulima wa miwani. Miradi hii ilichaguliwa kutoka kwenye orodha ya mamia ya maombi yaliyopokelewa, kwa sababu jamii zilizohusika zimedhihirisha nia thabiti na matayarisho mazuri ya kuboresha hali ya maisha ya wakazi wake.

Kwenye sherehe hiyo ya kutia saini mikataba ya miradi itakayofadhiliwa na mfuko wa ASSHF, Balozi Retzer alitoa hundi kwa wawakilishi wa vikundi kutoka: Bumbuli, Lushoto mkoani Tanga; Bagamoyo na Mafia mkoani Pwani; Dar-es-Salaam; Moshi na Usangi mkoani Kilimanjaro; Sumbawanga mkoani Rukwa; Pemba; Monduli mkoani Arusha; Karagwe mkoani Kagera, na Tarime mkoani Mara.

Huko Tanga, Shule ya Sekondari ya Bumbuli ilipewa Tshs.11,938,500 kujenga bweni la wasichana, bafu pamoja na nyumba ya mlezi wa bweni (matron). Mradi huu utajenga mazingira muafaka na salama kwa wanafunzi kujifunza. Huko Mafia, chama cha maendeleo cha Chole, Chole Society for Social Development kilipatiwa Tshs.7,832,400 kuwasaidia kunua vifaa vya tiba ya meno vitakavyotumiwa kwa jamii nzima inayoishi katika kisiwa hicho.

Chama cha kutunza mazingira cha Kaengesa wilayani Sumbawanga, Kaengesa Environmental Conservation Society (KAESO) kilipewa Tshs.6,125,810 kunuua miche ya miti na vifaa vya kuendeshea bustani katika eneo ambalo karibu miti yote imekwisha kukatwa. Mradi huo unazingatia utunzaji wa mazingira. Kikundi cha utunzaji mazingira cha Lepaje, Moshi, Lepaje Environment Group, kimepatiwa Tshs.4,085,500 zitazotumiwa kunuua miche katika kijiji cha Kifuni Juu, eneo ambalo linakabiliwa na tishio la kuwa jangwa. Msaada huo utatumiwa kupanda miti na kuwahamasisha wanakijiji kuendeleza bustani za miti. Kikundi cha Lepaje pia kitachukua jukumu la kutoa mafunzo kwa jamii kuhusu utunzaji wa misitu na mazingira.

Huko Bagamoyo, kikundi cha ulimaji wa miwani cha Msichoke, Msichoke Seaweed Farming Group, kimepatiwa Tshs.11,092,572 kununua mitumbwi na nyenzo za kilimo cha miwani. Kikundi hicho kina wanachama 58, kati yao wanawake ni 47. Mfuko wa maendeleo wa Kiromo, Kiromo Development Foundation utatoa mafunzo kwa wakulima juu ya mbinu za uzalishaji na masoko.

Miradi miwili ilichaguliwa wilayani Tarime. Kikundi cha maendeleo cha wanawake cha Mwanyangi, Mwanyangi Women Development Group, kilipatiwa Tshs.5,061,000 kupanua shughuli zao za kilimo na kunua pampu ya maji. Faida ya mradi huo itatumiwa kutoa ajira zaidi katika eneo hilo. Mradi mwingine ni mradi wa wanawake OBDC Women Initiative Project ambao umepewa Tshs.4,568,500 zitakazotumiwa kununua mashine ya kusaga ili wananchi waweze kupata lishe iliyo safi.

Huko Pemba, mradi wa kuendesha kivuko kisiwani Kojani, Kojani Ferry Project umepewa kiasi cha Tshs.5,950,000 kunua boti pamoja na injini iliyotengenezwa upya, ili kuwasaidia wanawake na watoto wanaoishi kisiwani humo kuwa na usafiri salama wa kwenda Likoni. Boti hii itakuwa ni msaada mkubwa kwa wanawake wanaovuka kuchota maji na kwa wanafunzi wanaohudhuria Shule ya Sekondari ya Likoni.

Mradi wa maji wa Rirayo Kwanguma huko Usangi, wilayani Mwanga umepewa Tshs.6,136,200 kuwasaidia kujenga tanki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa ujazo wa mita 45 ambalo litaziwezesha familia 100 kupata maji safi na salama. Kikundi hicho tayari kinatoa huduma ya maji kwa familia 412.

Chama cha ushirika cha wakulima cha Nguvumali wilayani Karagwe, Nguvumali Farmer's Cooperative Society kimepewa Tshs.4,568,500 kuwasaidia kulima shamba la ekari 20 za miti ya mbao na kahawa. Shamba hili linaweza kutumiwa kama dhamana ya kujipatia mikopo kwenye taasisi za fedha hapa nchini.

Mkoani Arusha, kikundi cha wafugaji cha Ilkisongo, Ilkisongo Pastoralists Initiative, kilicho wilayani Monduli kimepewa Tshs.6,120,000 ambazo zitatumiwa kununua madawati kwa shule tatu za msingi katika eneo hilo. Wanafunzi wa shule za msingi ndio watakaonufaika na mradi huo kwa sababu utawajengea mazingira bora ya kujifunza.

Mradi mwingine uko jijini Dar es Salaam kwenye shule ya chekechea ya Mt. Moses iliyo Yombo Vituka, ambayo imepewa Tshs.6,111,085 zitakazotumiwa kujenga choo za wanafunzi, tanki la kuhifadhi maji, pamoja na uzio kuzunguka shule. Hii italeta mazingira safi na salama kwa wanafunzi.

- Translation -
This content is also available in English