| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Mpango wa PEPFAR watoa dola milioni 25 kusaidia mradi wa “UJANA” kuhamasisha vijana kujikinga na UKIMWI
Septemba 18, 2006
Mpango wa Rais wa Marekani wa kupunguza makali ya UKIMWI (PEPFAR), kupitia shirika la misaada la Marekani USAID umetoa kiasi cha dola milioni 25 kusaidia shughuli za kuzuia maambukizi ya UKIMWI miongoni mwa vijana nchini Tanzania. Mradi huo wa miaka mitano unaoitwa UJANA utatekelezwa na shirika linalojishughulisha na masuala ya afya ya kifamilia - Family Health International (FHI). Taasisi tatu kutoka Tanzania, African Medical and Research Foundation (AMREF), Femina/Health Information Project na TRACE OD (Organizational Development Training and Facilitation Center) zitasaidia kuutekeleza mradi huo hapa nchini. Takriban taasisi 50 hapa nchini zinaweza kupata sehemu ya msaada huo.
UKIMWI ni janga la kitaifa linalotishia afya za wananchi wa Tanzania na uchumi wao. Takriban asilimia 60 ya maambukizi mapya yanatokea miongoni mwa vijana, huku wasichana na vijana wanawake wakiathrika na kuwa hatarini zaidi. Vijana wengi nchini Tanzania wanafahamu kuhusu UKIMWI, ingawa hawana ujuzi na staidi za kujikinga.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, mradi wa UJANA utawasaidia vijana kubadili tabia zao na kupata stadi ambazo zitawawezesha kujikinga na UKIMWI. Mradi wa UJANA utafanya kazi na watu wazima wenye ushawishi katika jamii, pamoja na jamii nzima kuwasaidia vijana kujizuia, au kuahirisha kufanya mapenzi; kuwa waaminifu kwa mpenzi mmoja; kupunguza idadi ya wapenzi, au kama inafaa, kutumia kinga ya kondomu. Mradi wa UJANA utatoa uongozi wa kifundi na uratibu ili kusaidia kusambaza matokeo ya utafiti kuhusu mikakati inayofaa zaidi. Mradi wa UJANA pia utawapa vijana fursa ya kupata huduma mbalimbali za kijamii na ushauri nasaha. Mradi huo pia utasimamia kampeni ya ISHI, ambayo ni kampeni ya kitaifa ambayo inahamasisha vijana kujikinga na UKIMWI.
Mwenyekiti Mtendaji wa TACAIDS Meja Jenerali (msataafu) Lupogo alisema, “Serikali ya Tanzania inaukaribisha mradi huu mpya wa kuzuia maambukizi miongoni mwa vijana wa Tanzania, na tunafurahi kwamba mradi wa UJANA utatumia uwezo wa taasisi zilizopo hapa hapa nchini.”
Mkurugenzi wa shirika la misaada la USAID Pamela White alisema, “Wasichana na vijana wanawake hasa ndio wanaoathirika zaidi na janga hili. Mlengo wa mradi wa UJANA kwenye masuala ya jinsia ni muhimu kwa mustakabali wa wasichana na wavulana, wanawake na wanaume wa Tanzania. Kwa kufanya kazi pamoja na Serikali ya Tanzania, tunajua tunaweza kuleta tofauti.”
Jina la mradi – UJANA linaonyesha nguvu na moyo wa vijana, huku kila herufi ikisimamia baadhi ya falsafa za mradi huu: Ustadi, Juhudi, Ari, ni Nguzo za Afya.



