Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Bodi ya Wakurugenzi ya taasisi ya Serikali ya Marekani ya Millennium Challenge Corporation yaidhinisha msaada wa kupunguza umaskini Tanzania wa dola milioni 698

Septemba 18, 2007

Washington, D.C.— Bodi ya Wakurugenzi ya taasisi ya Serikali ya Marekani ya Millennium Challenge Corporation (MCC), imeidhinisha msaada wa miaka mitano wa kiasi cha dola milioni 698 wenye lengo la kupunguza umaskini, kuchochea kukua kwa uchumi, na kuongeza kipato cha jamii kupitia uwekezaji katika miundombinu ya sekta za usafiri, nishati, na maji.

“Mkataba huu ni ushahidi tosha wa juhudi za dhati za Watanzania kujijengea wenyewe maisha bora na pia kwa watoto wao,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa MCC, Balozi John Danilovich. Danilovich alitembelea Tanzania mwishoni mwa mwezi Januari na kukagua sehemu mbalimbali zilizopendekezwa kwa utekelezaji wa miradi, na kusisitiza umuhimu wa kuanzisha kitengo madhubuti cha kudhibiti masuala ya fedha (Financial Intelligence Unit) nchini Tanzania. Kufuatia idhini ya bodi ya MCC, Danilovich alisema, “Taasisi ya MCC inawapongeza wananchi wa Tanzania kwa kuandaa mpango kabambe uliolenga kushughulikia vikwazo muhimu vinavyokwamisha kukua kwa uchumi wa Tanzania – mtandao dhaifu wa usafiri, huduma ya nishati ambayo haiaminiki na wala haikidhi mahitaji, na upungufu wa maji safi na salama. Miradi hii ya uwekezaji katika kuboresha sekta za usafiri, nishati, na maji, ambayo imechaguliwa na Watanzania wenyewe - itakuwa ni chachu ya kupunguza umaskini na kuchochea ukuaji wa uchumi.”

Msaada wa taasisi ya MCC utakaotumiwa kukarabati barabara za Tanzania utasaidia kuwaunganisha watumiaji wa barabara pamoja na jamii, na masoko, shule, vituo vya fya, na pia kuimarisha upanuaji wa fursa za kiuchumi, kupitia kushuka kwa gharama za usafirishaji. Uwekezaji katika nishati inayoaminika ni muhimu kwa shughuli za sekta binafsi, na pia katika kuwapa Watanzania huduma za kijamii kama vile elimu na afya. Msaada huo pia unafadhili uboreshaji wa miundombinu ya maji, ambao utaongeza upatikanaji wa maji na kupunguza kutokea kwa maradhi yanayohusiana na maji; kupunguza gharama kubwa za tiba; na kudhibiti kushuka kwa tija miongoni mwa wafanyakazi.

Balozi Danilovich aliongozea kwamba, “Kupitia msaada huu wa Millennium Challenge, wananchi wa Marekani wanaona fahari kusaidia juhudi za Tanzania katika kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wananchi wake. Ninampongeza Rais Kikwete kwa uongozi na msaada wake katika kipindi chote cha kuandaa mkataba huu.

Utiaji saini wa mkataba huu unategemea mafungu ya mwaka wa fedha wa 2008. Baada ya mkataba huo kutiwa saini, msaada wa Millenium Challenge kwa Tanzania utakuwa ni mkubwa kuliko yote katika historia ya taasisi ya MCC. Tangu ianzishwe mwaka 2004, taasisi ya MCC imeidhinisha mikataba ya thamani inayozidi jumla ya dola bilioni 5.5 kwa nchi 16: Madagascar, Cape Verde, Honduras, Nicaragua, Georgia, Armenia, Vanuatu, Benin, Ghana, Mali, El Salvador, Mozambique, Lesotho, Morocco, Mongolia, na sasa Tanzania.

Taasisi ya Millennium Challenge Corporation (MCC), ambayo ni shirika la Serikali ya Marekani, lenye lengo la kufanya kazi na nchi maskini kabisa duniani, linaendeshwa kwa msingi kwamba, misaada inazaa matunda zaidi kama inaimarisha utawala bora, uhuru wa uchumi, na uwekezaji katika wananchi, ambao unasaidia kukuza uchumi na kutokomeza umaskini uliokithiri.