Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Balozi wa Marekani atembelea miradi inayofadhiliwa na mpango wa PEPFAR kwenye hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar

September 19, 2005


Balozi wa Marekani nchini Michael L. Retzer alimtembelea kwa mara ya kwanza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mheshimiwa Salum Juma Othman Jumatatu Septemba 19, 2005. Baada ya kufanya ziara fupi ya ofisi za Wizara hiyo, Balozi na Waziri walielekea kwenye hospitali ya Mnazi Moja kukagua miradi ya kupambana na UKIMWI ambayo inafadhiliwa na mpango wa dharura wa Rais Bush wa kupunguza makali ya janga la UKIMWI, President's Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR).

Balozi Retzer na Waziri Othman, wakifuatana na maafisa wa Ubalozi na Wizara walitembelea miradi mitatu kwenye hospital hiyo inayofadhiliwa na mpango wa PEPFAR na kutekelezwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ikishirikiana na taasisi ya Marekani ya kudhibiti magonjwa - U.S. Centers for Disease Control (CDC).

Kliniki za Mnazi Mmoja zinazotoa huduma ya afya kwa mama na mtoto zilianza kufanya kazi Aprili mwaka huu na zinatoa huduma za ushauri na kupima UKIMWI kwa mama wajawazito; utoaji wa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI; ushauri juu ya lishe ya watoto wachanga; na kuwapeleka wanawake walioonekana kuwa na virusi vya UKIMWI kwenye kliniki inayotoa huduma za matunzo na tiba (Care and Treatment Clinic). Mkurugenzi Mkazi wa taasisi ya CDC nchini, Stephan Wiktor, ambaye alikuwa kwenye ziara hiyo anakadiria kwamba zaidi ya mama wajawazito 1038 wamepata huduma za msingi za kliniki za kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, pamoja na huduma za ushauri na kupima.

Kituo cha pili cha ziara hiyo kilikuwa ni kliniki ya kutoa huduma za matunzo na tiba (Care and Treatment Clinic) ambayo ilianzishwa Juni 2005. "Kliniki hii inatoa huduma za uchunguzi na kupima; ushauri juu ya matumizi sahihi ya dawa; utoaji wa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI, antiretrovirals (ARVs) kwa wagonjwa wanaostahili; pamoja na ufatiliaji wa karibu wa hali ya wagonjwa hao," alisema Wiktor. Aliongeza kwamba, kati ya waathirika 300 walioandikishwa kwenye kliniki hiyo, 83 wanapata tiba ya dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs).

Balozi Retzer na Waziri Othman pia walitembelea maabara ya kisasa ya UKIMWI iliyo Mnazi Mmoja ambayo inaongoza katika kufanya tafiti juu ya kuenea kwa magonjwa ya zinaa (STDs). Wiktor alisema, "kupitia msaada wa PEPFAR, maabara hiyo mpya inafanya vipimo zaidi ya 300 vya kubaini virusi vya UKIMWI; vipimo 120 vya baiokemia na vipimo 120 vya kuhesabu chembe chembe za damu, kila mwezi."

Wiktor aliongezea kwamba, uwezo wa kufanya vipimo hivyo ni wa muhimu sana katika juhudi za kupambana na janga la UKIMWI kwa sababu unabainisha ni watu gani wameathirika na virusi vya UKIMWI, na ni wagonjwa gani wanaweza kufaidika zaidi na tiba. Vipimo hivyo pia vinatoa tathmini ya ufanisi wa tiba wanayopata wagonjwa.

Balozi Retzer aliwaambia waandishi wa habari waliofuatana naye katika ziara hiyo kwamba, mpango wa PEPFAR unatoa takriban Sh. bilioni 90 kwa mwaka kuisaidia Tanzania katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Alisema kuwa vitengo kadhaa vya Ubalozi, ikiwemo taasisi ya CDC na shirika la misaada la USAID vinashirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Zanzibar kuhakikisha kwamba rasilimali zinazotumiwa zinashughulikia mahitaji ya wananchi wa Zanzibar.

"Nilifurahi sana kuona rasilimali hizi za Kimarekani zikifanya kazi ya kutoa huduma za kuokoa maisha ya binadamu na kuwapa dawa mama wajawazito na watoto wao. Nina shauku kuendeleza ushirikiano wa karibu na Waziri, pamoja na maafisa wake katika kuimarisha juhudi za kuzuia maambukizi ya UKIMWI, pamoja na huduma za tiba na matunzo Visiwani Zanzibar.

- Translation -
This content is also available in English