Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Balozi wa Marekani apongeza kuidhinishwa kwa mkataba wa msaada wa Millennium Challenge

Septemba 19, 2007

Balozi mpya wa Marekani nchini, Bwana Mark Green, amepongeza tangazo lililotolewa September 18, 2007 na Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi ya Millenium Challenge Corporation (MCC) kuhusu kuidhinishwa kwa msaada wa dola milioni 698 (Sh. bilioni 872.5) kusaidia mikakati ya kupunguza umaskini nchini Tanzania.

"Ni heshima kubwa kwangu kuwasili Dar-es-Salaam kama Balozi mpya wa Marekani kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati huu ambao mkataba wa msaada mkubwa kuliko yote katika historia ya taasisi ya MCC ukiwa katika hatua za mwisho za kufanyiwa kazi. Nilipokuwa Mbunge wa Baraza la Congress, nilisaidia kuandika mswada wa kuanzishwa kwa mfuko wa Millennium Challenge. Sasa hivi nina shauku ya kushuhudia utekelezaji wa miradi ambayo pindi itakapokamilika, itahakikisha kiwango bora cha maisha kwa Watanzania wote.”

Balozi Green alisema kwamba, inawezekana maneno ya “MCC” na “Mswada wa Millennium Challenge” mwanzoni yakawachanganya watu wengine, lakini hivi karibuni watu watajifunza jinsi mpango huu unavyoweza kuleta tofauti kubwa katika maisha ya Watanzania.

“Mkataba mpya wa MCC utakapotiwa saini na Serikali ya Tanzania, utajenga ushirikiano wa karibu kati ya mataifa yetu mawili,” alisema. “Huu si msaada peke yake, bali ni juhudi kati ya Wamarekani na Watanzania kukabiliana na changamoto muhimu kama vile kuboresha barabara na nishati ya umeme. Msaada huu pia unaweka mkazo mpya kwenye uwazi pamoja na vita dhidi ya rushwa.”

Balozi Green aliongezea, “Nitakuwa nikijadili masuala yanayohusiana na taasisi ya MCC na wananchi nitakaokutana nao nchini kote Tanzania, na jinsi gani ninaweza kuhamasisha mabadiliko zaidi.” Msaada wa taasisi ya MCC uliotolewa na wananchi wa Marekani ni mpango wa miaka miaka mitano, wenye lengo la kupunguza umaskini, kuchochea kukua kwa uchumi, na kuongeza kipato cha jamii, kupitia uwekezaji katika miundombinu ya sekta za usafiri, nishati na maji, nchini kote Tanzania.

Alipokuwa Mbunge wa Baraza la Congress, Balozi Green siyo tu kwamba alisaidia kuandika mswada huo mpya, bali alikusanya kura zilizokuwa zinahitajika kuupitisha mswada huo. Balozi Green alisema kwamba, sasa anataka kusaidia kuongoza juhudi za kuufanya mkataba huu wa MCC ufanikiwe kuliko yote ulimwenguni.