Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Balozi wa Marekani atembelea miradi ya elimu Visiwani Zanzibar inayofadhiliwa na USAID

Septemba 20, 2005


Balozi wa Marekani nchini Michael L. Retzer alimtembelea kwa mara ya kwanza Waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman Jumanne Septemba 20, na kufanya ziara fupi ya ofisi za Wizara hiyo ambako alikutana na maofisa waandamizi wa Wizara.

Baadaye Balozi Retzer na Waziri Suleiman walitembelea vituo viwili vya miradi ya elimu inayopata ufadhili kutoka shirika la misaada la Marekani USAID, kupitia Mpango wa Kuboresha Elimu Zanzibar (MKEZA). Vituo hivyo viwili ni vile ambavyo vilitembelewa na mke wa Rais Bush alipozuru Zanzibar mwezi wa Julai: Kituo cha Al-Rahma Madrasa pamoja na Kituo cha Waaalimu, Shule za Msingi na Sekondari, Kiembesamaki. Kwenye vituo vyote viwili, Balozi na Waziri waliongea na wanafunzi, waalimu na maofisa utawala wa shule hizo.

Kituo cha Waalimu cha Kiembesamaki ni mradi wa USAID wa kuboresha taaluma ya ualimu, Teacher Advancement Programme (TAP) na kinatoa shahada ya juu kwa waalimu wa sekondari, Advanced Secondary Teaching Certificate.

Mpango huu wa miaka miwili ulipokea kwanza kiasi cha zaidi ya bilioni 4 kutoka shirika la USAID kuboresha elimu Visiwani Zanzibar kwa kujenga ushirikiano wa karibu kati ya vikundi vya jumuiya na serikali, kuanzia chekechea mpaka shule za sekondari. Mpango huu unagusa karibu kila sekta ya mfumo wa elimu Zanzibar. Mpango huu unaotekelezwa na taasisi ya Aga Khan, Aga Khan Foundation, kwa niaba ya shirika la USAID, unahusisha pia vikundi vinavyoishi katika mazingira magumu, kwa mfano walemavu na wasichana.

Bwana Thomas Bayer wa shirika la USAID, aliyekuwa kwenye ziara hiyo alisema kwamba, tangu uzinduzi wa mpango wa MKEZA, shughuli nyingi zimefanikishwa Visiwani Zanzibar. Alisema orodha ni ndefu, lakini shughuli hizo ni pamoja na: kuboresha vituo tisa vya waalimu; kukamilisha ujenzi wa shule katika maeneo 18 (10 Unguja na 8 Pemba); kununua vitabu vya hesabu, sayansi na vifaa vya maabara kwa vijana wa Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu, Utamaduni na Michezo; pamoja na maandalizi ya kozi mpya ya juu kwa waalimu wa sekondari, Advanced Secondary Teachers Certificate (ASTC) ili kuwapandisha waalimu wa shule za msingi wafikie kiwango cha waalimu wa sekondari, ambao wanahitajika sana.

Aidha, Bayer aliongezea, mpango wa MKEZA ulifadhili ziara ya wiki mbili ya mafunzo ya Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Marekani, ambao walitembelea taasisi za elimu nchini Marekani kujifunza masuala ya sera na mbinu za kuboresha elimu Zanzibar. Mpango huo pia ulifadhili washiriki 160 kutoka Pemba na Unguja kuhudhuria warsha maalum iliyochochea mwamko kuhusu mahitaji ya suala hili muhimu; na pia ulifadhili asasi 10 zisizo za kiserikali kuandaa mpango wa kuimarisha elimu kwa wasichana.

Balozi Retzer aliwaambia waandishi wa habari waliofuatana naye katika ziara hiyo kwamba, amefurahi sana kuona juhudi thabiti zinazofanywa na shirika la USAID kuimarisha sekta ya elimu Visiwani Zanzibar. Alisema, "ni muhimu sana kwa jamii yoyote kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata elimu nzuri, na mimi nimefurahi kuona kwamba Wizara na vikundi vinavyosaidiwa na shirika la USAID hapa Zanzibar vinachangia msimamo wetu thabiti kufanikisha zoezi hili. Ninajivunia mafanikio yaliyofikiwa, na nina shauku kuendeleza kasi ya utekelezaji wa miradi hii ili kuboresha zaidi sekta ya elimu hapa Zanzibar."

- Translation -
This content is also available in English