Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Mpango wa T-MARC wa shirika la misaada la USAID wazindua aina mpya ya kinga za kuzuia mimba ili kukabiliana na changamoto zinazohusu afya ya wanawake

September 22, 2005


Leo ni siku ya uzinduzi wa zana mbili zinazohusu afya ya uzazi kwa wanawake: Vidonge vya kuzuia mimba na kondomu za kike. Uzinduzi huo utakaofanyika jijini Dar-es-Salaam utawaelimisha serikali, sekta binafsi, asasi zisizo za kiserikali, vyombo vya habari na wafadhili kuhusu zana hizo mpya ili kuhamasisha utangazaji na usambazaji wa zana hizo nchini kote. Katika wiki zijazo kutakuwepo na tamasha na shughuli mbalimbali za kuelimisha na kuhamasisha umma ambazo zitafanyika kwenye maeneo yanayotembelewa zaidi na wanawake, kama vile saluni, kliniki, na hata kitchen party. Shughuli hizi zitawalenga watumiaji watarajiwa wa zana hizi - wanawake waliofikia umri wa kuzaa na makundi yaliyo hatarini kuambukizwa - nchini kote.

Vidonge vya kuzuia mimba vitawapa wanawake wanaotaka kupanga uzazi njia rahisi na thabiti ya kufanya hivyo. Kondomu za kike zinatoa njia mbadala ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa - njia ambayo inampa mwanamke uhuru wa kuamua matumizi yake, tofauti na hali ilivyo katika matumizi ya kondomu za kiume. Jumbe zitakazotumika katika promosheni ya zana hizi ni: "Uhuru wa kupanga" pamoja na "Huru na Raha - Jiamulie," Zana zote mbili zitawawezesha wanawake kulinda afya zao na zile za watu wanaowapenda.

Ni asilimia 28 tu ya wanawake wanaoishi katika ndoa wanaotumia njia za kisasa za kupanga uzazi. Kwa hiyo, kuna fursa kubwa ya kuongeza matumizi ya njia za kisasa za kupanga uzazi kupitia mbinu za kibiashara katika mauzo na usambazaji. Kwa kuwa kiwango cha maambukizi kwa wanawake ni kikubwa zaidi (asilimia 7.7) ukilinganisha na wanaume (asilimia 6.3), kondomu za kike ni muhimu katika kulinda afya za wanawake nchini Tanzania. Utafiti umeonyesha kwamba, kama kondomu za kike zitapatikana, matumizi ya kondomu kwa jumla yataongezeka.

Zana hizi zinazinduliwa na shirika la misaada USAID, mradi wa T-MARC (Tanzania Marketing and Communication for HIV/AIDS, Reproductive Health and Child Survival Project) . Mradi wa T-MARC unaendeshwa na taasisi ya kuendeleza elimu, Academy for Educational Development (AED). Lengo la mradi huu ni kuboresha afya ya wananchi wa Tanzania kupitia utoaji wa zana na huduma zenye bei rahisi kwa ajili ya kufanikisha mapambano dhidi ya UKIMWI na pia kuboresha afya ya watoto.

Vidonge hivyo vya kuzuia mimba vitauzwa chini ya jina la 'Flexi P' na kondomu ya kike chini ya jina la 'Lady Pepeta,' na kusambazwa na kampuni zenye uzoefu mkubwa: Shelys Pharmacuetical na Kays Hygiene Products. Zana hizi zinapatikana kwenye sekta ya biashara na Watanzania wote wanaweza kuzitumia. Vidonge vya Flexi P vinapatikana kwenye maduka ya dawa na kliniki binafsi zinazotoa huduma za afya kwa mama na mtoto kwa bei ya Sh. 150 kwa vidonge vya mwezi mmoja. Kondomu ya Lady Pepeta inapatikana kwenye taasisi zenye miradi ya kupambana na UKIMWI na katika maduka ya dawa yaliyo jijini Dar-es-Salaam kwa bei ya Sh. 100.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa T-MARC, Rosemary Mwakitwange, "Zana zote hizi mbili zinalenga kukabiliana na changamoto muhimu zinazohusu afya ya umma na zinapatikana kwa bei nafuu. Uuzaji wa vidonge hivi vya kuzuia mimba na kondomu za kike unazingatia uwajibikaji na uhuru wa mtu binafsi kuchagua, katika juhudi za kupambana na janga la UKIMWI. Zana zote mbili zinakidhi viwango vya ubora vya kimataifa, ili kuhakikisha kwamba wanawake wanaweza kuzitumia bila wasiwasi katika kupanga uzazi na kufanya ngono salama."

Shirika la misaada la USAID linawekeza zaidi ya dola milioni mbili katika zana hizi kwa miaka minne ijayo. Fungu hili litatumiwa kutoa ruzuku ili kuwawezesha wanawake wengi kununua zana hizo kwa bei nafuu. Fungu hilo pia litatumiwa katika shughuli za kuwaelimisha wanawake wa Tanzania juu ya umuhimu na matumizi sahihi ya zana hizi.

Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na

Bi. Prisca Rwezahura
Partnership/Co-operation Specialist
AED/T-Marc Project
Email: prwezahura@tmarc.or.tz

- Translation -
This content is also available in English