Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Ubalozi wa Marekani wakabidhi mradi wa maji wa Lengasti

  • Mradi utawaepusha wanawake adha ya kutembea km 24 kila siku kuchota maji
  • Septemba 21, 2006

    Ubalozi wa Marekani umekabidhi mradi wa maji wa kijiji cha Lengasti Alhamisi Septemba 21, 2006 kwenye sherehe iliyofanyika kijijini hapo, katika wilaya ya Simanjiro. Kaimu Balozi wa Marekani Purnell Delly alisimamia sherehe ya kukabidhi mradi huo ambao umefadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia mpango wa misaada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani - Department of Defence Humanitarian Assistance Progamme.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani, huu ni mradi mkubwa kuliko yote ambayo imewahi kufadhiliwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania. Mradi huo ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 313.5 unatoa huduma ya maji kwa watu zaidi ya 6,000 na mifugo yao 16,000, kupitia mfumo unaounganisha pampu, mabomba, na matanki. Mfumo huu unasafirisha maji kutoka kwenye chanzo kilicho umbali wa kilometa 20.

    Delly alisema kwamba mradi wa maji wa Lengasti una pampu inayosukuma maji kutoka kwenye chemichemi iliyo chini ya ardhi, ikisaidiana na pampu nyingine iliyowekwa katikati ya bomba hilo lenye urefu wa kilometa 20. Kuna ofisi mbili za wahudumu wa kituo cha pampu, sehemu sita za kuchotea maji, pamoja na matanki mawili yenye ujazo wa lita 90,000. “Hicho ni kiasi kikubwa cha maji. Kuna hori tatu ndefu zinazohakikisha kwamba ng’ombe nao wanapata maji ya kutosha,” alisema Delly.

    Alisema kwamba, kabla ya mradi huo, wanawake wa Lengasti walikuwa wakitumia masaa kumi kila siku kwenda kuchota maji umbali wa kilometa 24. Hali hii iliwafanya wakose muda wa kufanya shughuli zingine. “Ningependa kugusia suala la akina mama waliopo hapa. Ninafahamu kwamba wanawake na wasichana, bila kujali umri wao, ndiyo hasa wanaochota na kubeba maji. Kwa hiyo nina furaha kubwa sana kuzindua mradi huu siku ya leo, nikijua kwamba utapunguza mzigo wa kazi kwa akina mama hawa wachapa kazi. Utumieni mradi huu vizuri na muutunze vizuri pia. Pokeeni salamu za kheri kutoka kwa wananchi wa Marekani, na hasa kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani,” alisema Delly.

    Mradi huu wa maji umejengwa kwenye eneo ambalo linafahamika kwa matatizo yake ya maji. Kwa hakika mradi huu utaboresha shughuli za kilimo, utapunguza umaskini na kuboresha afya ya wanakijiji. Shirika la World Vision Tanzania lilichaguliwa kuutekeleza mradi huu wa maji.

    Kwenye sherehe ya uzinduzi huo, Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Kanali (msataafu) Anatory Tarimo; Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Khalid Mandia. Wengine walikuwa ni Mkurugenzi wa Taifa wa shirika la World Vision, Getachew W. Michael, Mkurugenzi wa Kanda wa World Vision, Mashimba Ndaki, pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Lengasti, Mzee Maningo Kutatoi.

    - Translation -
    This content is also available in English