Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Balozi wa Marekani Mark Green ashiriki kufuturu na wanakijiji wa Misugusugu
Septemba 26, 2007
Septemba 25, 2007 Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania, Bwana Mark Green, alitembelea Kibaha, kijiji cha Misugusugu, pamoja na kituo cha kulea watoto yatima cha Mwinyibaraka, ambacho ni sehemu ya Taasisi ya Kiislamu ya Mwinyibaraka, na kuungana na viongozi na wakazi wa eneo hili katika ibada ya kufuturu iliyokuwa imeandaliwa na taasisi hiyo.
Ubalozi wa Marekani ulitoa msaada wa fedha kwa Taasisi ya Mwinyibaraka kwa ajili ya futari ya kituo hicho kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan, na kwa futari ya jana usiku kwa jumuia yote.
Alipowasili kwenye kijiji cha Misugusugu, Kibaha, Balozi Green alipokelewa na mwenyekiti wa taasisi hiyo, Sheikh Issa Othman Issa, na mwalimu mkuu wa Kituo cha Mwinyibaraka, na kituo cha kulea watoto yatima, Ustadh Abdallah, pamoja na viongozi wengine wa tasisi na kijiji hicho. Baada ya utambulisho mfupi kuhusu shughuli za taasisi hiyo na malengo yake, Balozi Green aliweka shada la maua kwenye kaburi la Sheikh Ahmed Mohamed Msiba, mwenyekiti wa kwanza wa Taasisi ya Mwinyibaraka.
Taasisi ya Kiislamu ya Mwinyibaraka ilianzisha madrasa na kituo cha kulea watoto yatima mwaka 2002 katika kijiji cha Misugusugu, Kibaha. Bado wana matumaini ya kuanzisha kituo rasmi cha elimu.
Kwenye hotuba yake fupi baada ya kufuturu, Balozi Green aliwashukuru wanakijiji kwa kumkaribisha kijijini hapo. Balozi Green alisema matumaini ya watoto wa kijijini hapo yanafanana na yale ya watoto wake, na pia alisifia mapishi mazuri ya chakula - - akisema kwamba mhogo na vyakula vingine alivyovifurahia ni “vizuri sana!”




