| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa kwa vyombo vya habari
Shirika la USAID latoa dola 393,000 kusaidia mpango mpya wa kusindika korosho na kupanua masoko ya nje
Septemba 28, 2005
Shirika la misaada la USAID na Wizara ya Fedha wametia saini mkataba Septemba 26, 2005 wa kutolewa kwa msaada wa dola 393,000 zitakazotumiwa kuimarisha usindikaji wa korosho ghafi nchini Tanzania na kupanua soko la zao hilo katika nchi za nje.
Ili kufanikisha azma hii, shirika la USAID litasaidia kuimarisha juhudi za asasi isiyo ya kiserikali ya TechnoServe kutoka Marekani, ambayo imefanikisha kuanzishwa kwa ubia kati ya kampuni ya Olam International Limited, kampuni kubwa zaidi duniani inayojishughulisha na biashara ya zao hilo, wasindikaji wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Tanzania, ili kuboresha shughuli za ulimaji, usindikaji na uuzaji wa korosho. Juhudi hizo zitaimarisha usindikaji wa korosho hapa nchini, zitaongeza nafasi za ajira pamoja na mapato kutoka mauzo ya nje.
Katika mwaka uliopita, Serikali ya Tanzania imekuwa ikishirikiana na wasindikaji hapa nchini kuandaa na kutekeleza makubaliano ambayo yatatoa motisha utakaohusisha kupunguzwa kwa kodi na ushuru unaotozwa na serikali, pamoja na juhudi za dhati za wasindikaji kuimarisha shughuli zao hapa nchini. Lengo la makubaliano hayo ni kuongeza kiasi cha korosho zinazosindikwa nchini Tanzania kwa tani 10,000 za metriki kila mwaka kwa miaka mitano ijayo. Hii italeta ongezeko la nafasi 30,000 za ajira na kuongeza thamani ya korosho zinazouzwa nje kwa kiasi cha zaidi ya dola milioni 15 katika miaka mitano ijayo ya mkataba huo.
Kutokana na mkataba huo, kampuni ya Olam International na asasi ya TechnoServe zitaungana pamoja katika ubia unaoitwa Global Development Alliance, ambao lengo lake ni kuboresha tija kwa wakulima wadogo wadogo na hivyo kuongeza kiwango cha mapato kwa wananchi wanaoishi vijijini. Pia watafanya kazi na vyama vya wasindikaji ili kuongeza ubora na uwezo wa ushindani wa wasindikaji wakubwa na wale wa kati.
Kwa mujibu wa Bwana A. Shekhar, Mkurugenzi Mwandamizi wa kampuni ya Olam International Limited, "Ubia kati ya Olam na TechnoServe ni ushahidi wa msimamo wetu kuhusu ushirikiano endelevu. Kwa kushirikiana pamoja, tunatumaini kuunga mkono mipango inayoongozwa na Serikali na sekta ya viwanda kutafuta mbinu muafaka zitakazoziwezesha nchi za Kiafrika zinazozalisha korosho kuboresha kwa kiwango cha juu uwezo wa sekta hiyo, kwa faida ya wadau wote, wakiwemo wakulima na wasindikaji wadogo wadogo."
Korosho zilizosindikwa ni lishe bora na zina soko kubwa katika nchi za Ulaya na Marekani. Kwa sasa hivi, bara la Afrika linazalisha theluthi moja ya korosho ghafi ulimwenguni, zao ambalo linaingiza kipato kwa mamilioni ya wakulima wadogo wadogo, wengi wao wakiwa wanaishi vijijini katika mazingira yanayotawaliwa na uhaba wa rasilimali, mbinu duni za uzalishaji na umaskini uliokithiri.
Zaidi ya asilimia 80 ya korosho kutoka Afrika zinauzwa kama korosho ghafi huko India au Vietnam ambako husindikwa. Kwa hiyo, wakulima wadogo wadogo wa Kiafrika hubaki na soko dogo sana ambalo haliwaletei faida kubwa. Ikiwa korosho zitasindikwa barani Afrika, Waafrika wengi zaidi watapata ajira na pato la fedha za kigeni kwa nchi litaongezeka. Hata hivyo, kuna changamoto katika kuanzisha sekta ya usindikaji: Unahitajika uwekezaji katika miundombinu ya usindikaji, pamoja na utalaamu wa kuendesha mitambo hiyo. Itabidi mafunzo maalum yatolewe ili kuwawezesha wafanyakazi kupata ujuzi unaohitajika. Hivi vyote vinahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa serikali za mitaa.



