Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa kwa vyombo vya habari

Serikali ya Marekani kupitia shirika la misaada la USAID yatoa msaada wa ziada wa dola milioni 6.5 kusaidia vita dhidi ya UKIMWI

Septemba 30, 2005


Shirika la misaada la USAID na Wizara ya Fedha wametia saini mkataba Jumatatu Septemba 26, 2005 wa msaada wa ziada wa kiasi cha dola milioni 6.5 ambazo zitatumiwa kusaidia katika vita dhidi ya UKIMWI nchini Tanzania. Hizi ni fedha zilizokuwa zimebaki kutoka kwenye fungu la jumla ya dola milioni 44.2 zilizokuwa zimetengwa na shirika la USAID kusaidia katika vita dhidi ya janga hilo hapa nchini kwa mwaka wa 2005. Msaada huu utatumiwa kutekeleza mpango wa dharura wa Rais Bush wa kupunguza makali ya UKIMWI unaojulikana kama President George W. Bush's Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR). Hii ni sehemu ya mchango wa Serikali ya Marekani kusaidia mpango wa taifa wa kutoa tiba na matunzo kwa waathirika wa UKIMWI - HIV/AIDS National Care and Treatment Plan.

Ili kukabiliana na changamoto ya janga la UKIMWI, Rais Bush alitenga 2003 fungu la dola bilioni 15 kwa miaka mitano, huu ni mpango wa kimataifa ulio mkubwa zaidi kuliko yote katika historia ambao umewahi kutekelezwa na serikali moja kukabiliana na janga la ugonjwa mmoja. Tanzania ni moja ya nchi 15 zinazolengwa na mpango huo wa Rais Bush, ambao mafanikio yake ni pamoja na kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma za ushauri nasaha na upimaji; kupanuliwa kwa huduma za kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto; na kuboresha utoaji wa tiba ya kupunguza makali ya UKIMWI, anti-retroviral therapy (ART). Fedha hizi pia zimetumiwa kutengeneza mitandao ya kuwasaidia watu wanaoishi na ugonjwa wa UKIMWI, wakiwemo watoto.

Mpango wa Rais Bush unatoa fursa kwa shirika la misaada la USAID pamoja na taasisi zingine za Serikali ya Marekani zinazotekeleza mpango huo (Wizara ya Mambo ya Nje, huduma ya kujitolea ya Peace Corps, vituo vya kudhibiti magonjwa - Centers for Disease Control and Prevention, pamoja na Wizara ya Ulinzi) ya kupanua kwa kasi juhudi za kupambana na janga la UKIMWI nchini. Juhudi hizi zinahusisha kinga, tiba na matunzo kwa waathirika, ambao ni pamoja na watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Msaada unaotolewa na mpango wa PEPFAR ni nyongeza kwa misaada mingine inayotolewa na shirika la USAID kwa sekta ya afya ili kuboresha huduma za uzazi na afya ya mtoto na pia kuimarisha mabadiliko katika sekta ya afya. Kwa pamoja, misaada yote hii inafikia takriban dola milioni 57 kwa mwaka wa 2005.

- Translation -

This content is also available in English.