| - Translation - |
|
This content is also available in English. |
Taarifa kwa vyombo vya habari
Balozi wa Marekani atoa zaidi ya Sh. milioni 50 kusaidia miradi ya kutetea haki za binadamu
Oktoba 3, 2005
Jumatatu Oktoba 3, 2005 Balozi wa Marekani Michael Retzer alitoa zaidi ya Sh. milioni 50 kusaidia miradi miwili chini ya mfuko wa Ubalozi wa kujenga demokrasia na kutetea haki za binadamu, Democracy and Human Rights Fund (DHRF).
Kwenye sherehe iliyofanyika kwenye Ubalozi wa Marekani, Balozi Retzer alikabidhi hundi hizo kwa wawakilishi wa Tume ya Kutetea Haki za Binadamu na Utawala Bora - Commission for Human Rights and Good Governance (CHRAGG), pamoja na taasisi ya Word and Peace Organisation (WAPO).
Tume ya Kutetea Haki za Binadamu na Utawala Bora ilipokea msaada wa Shs. 27,428,625 zitakazotumiwa kununulia vitabu pamoja na vitabu vya CD vinavyohusiana na haki za binadamu, utawala bora, na haki katika utawala, ili kuwa na maktaba ya umma ya kisasa ambayo itaweza kutumiwa kwa urahisi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, vifaa hivi vitakuwa vya manufaa kwa taasisi nyingi zisizo za kiserikali ambazo zinashughulikia masuala ya kutetea haki za binadamu.
Kwa upande mwingine, sehemu moja ya msaada wa kiasi cha Shs. 23,320,089 uliotolewa kwa taasisi ya WAPO utatumiwa kuandaa vipindi vya redio kuhusu masuala ya kutetea haki za binadamu, wanawake na watoto. Sehemu nyingine itatumiwa kuchapisha vipeperushi kuhusu masuala ya kutetea haki za binadamu.
Mfuko wa Kujenga Demokrasia na Kutetea Haki za Binadamu unatoa misaada kwa taasisi hapa nchini kufadhili shughuli ndogo ndogo za muda mfupi, kwa lengo la kuimarisha demokrasia, kutetea haki za binadamu na kuhamasisha kuzingatiwa kwa utawala wa sheria nchini Tanzania.



