Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Watu wa Miono wapokea vyema Uzinduzi wa Maabara Mpya uliofanywa na Mama Kikwete na Mwakilishi wa Serikali ya Marekani
5 Oktoba, 2009
Miono, Mkoa wa Pwani: Hapo Jumapili tarehe 4 Oktoba 2009, maabara mpya ilizinduliwa katika Kituo cha Afya cha Miono, kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani. Uzinduzi huu ulifanywa kwa pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, Mama Salma Kikwete, Mwakilishi wa Ubalozi wa Marekani nchini Bi. Emily Shaffer na Bi. Amy Cunningham kutoka Kituo cha Kimataifa cha Huduma na Matibabu ya UKIMWI (ICAP) cha Chuo Kikuu cha Columbia. Maabara hii iliyoanzishwa kwa msaada kutoka kwa watu wa Marekani kwa kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania itatoa huduma za kimaabara kwa zaidi ya wakazi 65,000 wa kijiji cha Miono.
Ukarabati mkubwa wa jengo lililodumu kwa takriban miaka 29 ambalo liliwahi kuwa jiko la kituo hicho cha afya na kulifanya kuwa maabara ya kisasa yenye vifaa vyote muhimu ni hatua muhimu katika jitihada za pamoja kati ya watu wa Tanzania na watu wa Marekani katika kupiga vita VVU/UKIMWI na kujenga mfumo imara wa utoaji wa huduma bora za afya katika ngazi zote nchini. Hapo awali Kituo cha Afya cha Miono kililazimika kupeleka sampuli za wagonjwa waliohitaji vipimo katika maabara iliyo katika umbali za zaidi ya kilomita 80, Ukosefu wa maabara za kisasa kwa ajili ya upimaji wa VVU na maradhi mengine ni tatizo linalovikabili vituo vingi vya afya vilivyopo katika maeneo ya vijijini na kuwafanya watu wengi kuchelewa kupata matibabu yanayoweza kuokoa maisha yao kwani hulazimika kusubiri muda mrefu kabla hawajapata majibu ya vipimo vyao. Hivi sasa Kituo cha Afya cha Miono kinaweza kufanya vipimo vya kisasa kabisa katika siku zote za wiki. Huduma hii inakwenda sambamba na huduma za bure zinazotolewa na Kituo cha Ushauri Nasaha na Matibabu ya UKIMWI cha Miono ambazo ni pamoja na utoaji dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV), ushauri nasaha na upimaji, programu za kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda mtoto na huduma nyingine kwa akina mama wajawazito.
Katika hotuba yake, Mama Kikwete alisisitizia umuhimu wa huduma za maabara katika kulinda afya ya mama na mtoto,“Tanzania itakuwa bila UKIMWI pale tutakapoweza kuzuia maambukizi kwenda kwa kizazi kipya. Kwa kuwa na huduma bora za maabara itarahisisha kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto, kuwapima watoto na kubaini hali yao na hata kuwapa matibabu mapema. Wazazi tunawajibika katika kuhakikisha kuwa tunawatunza na kuwalinda vyema watoto wetu”.
Kwa mwaka mmoja sasa watu wa Marekani kwa kupitia ICAP wamekuwa wakitoa msaada wa vifaa, fedha na utaalamu kwa mkoa wa Pwani ili kuboresha miundombinu, maabara na huduma za kitabibu pamoja na kujenga uwezo wa watendaji katika mfumo wa utoaji huduma za afya ili waweze kutoa huduma bora za matibabu ya VVU/UKIMWI.
Msaada wa Maabara ya Miono ni sehemu ya msaada unaotolewa na Serikali ya Marekani kwa Tanzania. Hadi mwisho wa mwaka huu wa fedha, Marekani itakuwa imeipatia Tanzania zaidi ya Dola za Kimarekani 817 milioni kwa ajili ya kukabiliana na VVU/UKIMWI. Hii ni sehemu ya msaada rasmi wa Serikali ya Marekani kwa Tanzania wa zaidi shilingi za Kitanzania 750 bilioni.




