Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Mfuko wa kuimarisha demokrasia na haki za binadamu watoa msaada wa shilingi milioni 65.2

Utasaidia vikundi Dar-es-Salaam, Rombo na Pemba

Oktoba 26, 2006


Balozi Michael L. Retzer alikabidhi leo Alhamisi Oktoba 26, 2006 msaada wa shilingi 65,269,500 kutoka kwenye Mfuko wa Kuimarisha Demokrasia na Haki za Binadamu - Democracy and Human Rights Funds (DHRF) kusaidia miradi minne ambayo itanufaisha vikundi vilivyo Pemba, Rombo na Dar es Salaam. Mfuko wa DRF unahamasisha uimarishaji wa demokrasia, utetezi wa haki za binadamu pamoja na uzingatiaji wa utawala wa sheria nchini Tanzania.

Miradi minne ambayo ilipokea misaada hiyo ni: Kikundi cha kutetea wanawake Afrika - Advocacy for Women in Africa (AWA), sh. 23,317,000; kikundi cha Akina Mama Jiendeleze Sote (AJISO), sh. 16,750,000; kikundi cha kujenga matumaini - Tanzania Hope (TANHOPE), sh. 11,522,500; pamoja na mtandao wa mawasiliano ya injili - Gospel Communication Network of Tanzania (GCNT/CLDP), sh.13, 680,000.

Kikundi cha Advocacy for Women in Africa kitaendesha warsha kisiwani Pemba itakayohusisha wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa ili kupunguza tofauti kati yao, kuimarisha ujuzi katika kupanga mipango, utetezi, na kutoa maamuzi. Lengo la muda mrefu ni kuongeza uwezo wa wanawake wa Pemba kuanzisha shughuli za kiuchumi ili kutokomeza umaskini na kuboresha ujuzi wao katika maeneo mengine.

Kikundi cha SOTE, ambacho kinajishughulisha na masuala ya amani na haki katika jamii na kuhudumia wananchi 30,220 kwenye vijiji vinane wilayani Rombo, kitatoa elimu kuhusu haki za binadamu, jinsia, ushirikishwaji wa jamii, elimu ya uraia, pamoja na uanzishaji na uimarishaji wa vikundi vya sheria vya wanawake. Vikundi hivyo vitatoa huduma za kusuluhisha migogoro katika juhudi za kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto.

Kikundi cha TANHOPE kitatoa mafunzo kwa wakufunzi ambao watawahamasisha wananchi kushiriki katika kuimarisha utawala bora katika jamii. Kikundi cha TANHOPE kitafafanua umuhimu wa demokrasia na jinsi inavyofanya kazi, na pia kubainisha vizuizi vya kushamiri kwa demokrasia.

Mtandao wa GCNT/CLDP utajishughulisha na kutetea haki za watoto, kupambana na magonjwa, umaskini, ujinga, na pia kuiwezesha jamii kufanya kazi pamoja kuimarisha maisha ya kiroho – ikiwa ni pamoja na majukumu ya kutoa misaada kwa jamii.

Akiongea wakati wa sherehe iliyofanyika kwenye Ubalozi wa Marekani, Balozi Retzer alisema, “Miradi inayofadhiliwa na mfuko wa DHRF nchini Tanzania inaongeza mwamko katika masuala ya haki za binadamu, raia na siasa kupitia kampeni zinazotekelezwa katika ngazi za mitaa na taifa. Mfuko huo unalenga kupanua wigo wa kutoa elimu ya haki za sheria na kuongeza fursa ya wanawake kufaidika na mfumo wa sheria.”

Msaada huu unafanya jumla ya misaada iliyotolewa na Mfuko wa Kuimarisha Demokrasia na Haki za Binadamu - Democracy and Human Rights Fund (DHRF) kufikia zaidi ya shilingi milioni 400 ($335,914), tangu ulipoanzishwa 2000.

- Translation -
This content is also available in English