Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Press Releases > Tanzania kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Marekani na Afrika Wanaoshughulikia Masuala ya Usafiri wa Anga utakaofanyika huko Atlanta
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Tanzania kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Marekani na Afrika Wanaoshughulikia Masuala ya Usafiri wa Anga utakaofanyika huko Atlanta

Mkutano unatarajiwa kuweka msisitizo zaidi katika miradi ya uendelezaji wa miundombinu

26 Oktoba 2009

ATLANTA – Mawaziri kutoka nchi kumi za Kiafrika leo wanaanza mkutano wa siku nne utakaowakutanisha na Wizara, idara na taasisi mbalimbali nchini Marekani ikiwa ni pamoja na Wizara ya Biashara na Maendeleo, Idara ya Usafirishaji, Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Anga na Jumuiya ya wafanya biashara wa Marekani waliodhamiria kuimarisha uhusiano wa kibiashara unaoelenga kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa anga na kugharimia miradi ya maendeleo ya sekta hii na usalama wa anga. Mkutano huu utajadili changamoto kuu kuhusu miundombinu ya usafirishaji wa anga zinazozikabili nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unajumuisha watu wanne, wakiongozwa na Waziri wa Miundombinu Dk. Shukuru Kawambwa. Wajumbe wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Prosper Tesha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Tanzania, Margaret Munyagi na Afisa Mwandamizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Anga, Ladislus Matindi.

Katika kuunga mkono mkutano huu, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hartsfield-Jackson uliopo Atlanta utawaandalia wajumbe kutoka Afrika na wale wa Marekani ziara ya kutembelea uwanja huo ili kujionea utendaji wake. Uwanja huu umebuniwa kipekee ukiwa na njia za kurukia na kutua ndege zinazokwenda sambamba (parallel runway design), jambo linalofanya uwanja huu uweze kutambulika duniani kutokana na ufanisi wake. Mawaziri wengine wanaohudhuria mkutano huu wanatoka katika nchi za Burkina Faso, Ghana, Kenya, Liberia, Mali, Namibia, Nigeria, Uganda na Zambia.

Aidha, washiriki watapata fursa ya kuona miradi muhimu ya uendelezaji wa viwanja vya ndege na katika kushiriki katika mawasilisho ya mada kuhusu miradi ya upanuzi wa viwanja vya ndege ikiwa ni pamoja na miradi ya uboreshaji wa maeneo ya viwanja ya kuwahudumia abiria (terminal modernization projects) na upanuzi ili kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo.

Mbali na mawasilisho hayo, washiriki watapata pia fursa ya kujadiliana kuhusu ugharimiaji wa miradi ya uendelezaji wa sekta ya anga na mikakati ya kubainisha vyanzo vya fedha kwa ajili ya kugharimia uboreshaji wa viwanja na sekta nzima ya usafirishaji wa anga.

Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Marekani inalenga katika kuinua maendeleo ya kiuchumi na maslahi ya kibiashara ya Marekani katika nchi zinazoendelea na zile zenye kipato cha kati (middle-income countries). Wizara hii hutoa misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na misaada ya kiufundi, upembuzi yakinifu, mafunzo, warsha zinazolenga katika kuboresha miundombinu ya biashara na kuweka mazingira ya kibiashara ya haki na uwazi. Mkakati wa Wizara hii wa kutoa misaada kwa nchi mbalimbali ili kusaidia katika kuweka sera nzuri za uwekezaji na ufanyaji maamuzi huzisaidia nchi hizo kujenga mazingira mazuri yatakayowezesha biashara, uwekezaji na maendeleo endelevu. Katika kutekeleza azma yake, Wizara ya Biashara na Maendeleo huweka msisitizo katika sekta za uchumi zinazoweza kunufaika kutokana na bidhaa na huduma kutoka Marekani.

 
Article translated in: