Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Msaada wa Fedha kukabiliana na Athari za Mgogoro wa Kiuchumi Duniani: Tanzania yapokea Dola za Kimarekani milioni 37.7 kutoka Marekani kwa ajili ya Kuchochea Ukuaji wa Uchumi
Naibu Waziri wa Fedha wa Marekani atangaza Msaada huu katika Mkutano wake na Rais Kikwete uliofanyika Jumatatu
Novemba 2, 2009
Toka kuanza kwa mgogoro wa kifedha wa kimataifa hali ya kiuchumi kwa mataifa mengi duniani imekuwa ngumu sana. Wakati ambapo mgogoro huu umeiathiri Marekani, bado watu wa Marekani wanaelewa kuwa athari zake kwa Tanzania ni kubwa zaidi. Ili kupunguza makali ya athari hizo, Rais Obama na Bunge la Congress la Marekani limeidhinisha “Mpango wa Kukabiliana na Athari za Kuporomoka kwa Uchumi” (Financial Crisis Initiative) utakaogharimu kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 37.7 utakaowanufaisha moja kwa moja watu masikini nchini Tanzania. Msaada huu ulitangazwa rasmi na Naibu Waziri wa Fedha wa Marekani Neal S. Wolin wakati wa mkutano wake na Rais Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam hivi leo.
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) unashirikiana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika kusimamia jitihada hizo. Ushirikiano huu unadhihirisha azma ya dhati ya Marekani ya kushirikiana na Umoja wa Mataifa na wafadhili wengine katika kusaidia jitihada za maendeleo za Tanzania.
"Marekani inafarijika sana kufanya kazi na nchi za Kiafrika zenye azma ya dhati ya kujiletea maendeleo kama Tanzania, kuzisaidia kuweza kuvuka kipindi hiki kigumu cha mgogoro wa fedha na kuanguka kwa uchumi wa dunia na hatimaye kuwa na ustawi katika miaka ijayo," alisema Naibu Waziri Wolin. "Tunatarajia kuimarika zaidi kwa ubia wetu na Tanzania katika maeneo na nyanja mbalimbali kutoka kuhamasisha maendeleo ya kilimo hadi kutoa misaada ya kitaalamu."
Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa wamekadiria kuwa athari za mgogoro wa kifedha dunia zitasababisha kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa zaidi ya asilimia 7 katika mwaka 2008 na kati ya asilimia 4 na 5 katika mwaka 2009. Ikiwa tayari zaidi ya Watanzania 40,000 wamepoteza ajira zao, ni wazi kuwa watu masikini ndio wanaoathiriwa zaidi na kuporomoka huku kwa uchumi. Kwa sababu hiyo mpango huu wa kuchochea ukuaji wa uchumi unamlenga moja kwa moja mwananchi na kuunga mkono jitihada za hivi sasa za Tanzania za kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini na kuongeza uzalishaji wa chakula.
Watoto ndio wanaoathiriwa zaidi na tatizo la upungufu wa chakula. Lishe bora mashuleni huwasaidia watoto kufanya vizuri zaidi katika masomo yao na kuzipunguzia mzigo familia zao kutokana na kupanda mno kwa bei za vyakula. Msaada huu utaiwezesha WFP kutoa milo miwili kwa siku kwa mwaka mzima kwa watoto 400,000 walio katika shule za msingi zipatazo 600 katika maeneo yaliyokumbwa na ukame katika mikoa ya Arusha, Manyara, Dodoma na Singida. WFP itatoa pia chakula kwa wanafunzi katika maeneo yaliyoathiriwa na kuporomoka kwa bei ya mazao na bidhaa za biashara kama vile pamba, maua, kahawa na vito vya thamani.
Mpango huu utasaidia pia kupunguza athari za kupungua kwa fursa za ajira kwa kutoa fursa za ajira za muda kwa maelfu ya Watanzania kutoka katika kaya masikini zaidi. Mpango huu wa kutoa ajira utalenga zaidi jamii za vijijini kwa kutoa ujira kwa wananchi watakaofanya kazi za kuboresha mifumo ya umwagiliaji na usambazaji wa maji safi, kupanda miti, kujenga maghala ya chakula na kukarabati barabara za vijijini. Katika jamii za wafugaji, mpango huu utasaidia ujenzi wa mabwawa, kuandaa maeneo maalumu ya malisho ya mifugo ili kuinenepesha na kuimarisha upatikanaji wa masoko.
Maeneo ya Usimamizi wa Wanyamapori yaliyoathirika kutokana na kupungua kwa mapato yatokanayo na utalii yatafaidika kwa kuanzishwa kwa vikosi maalumu vya uhifadhi (Conservation Corp). Wanavijiji wataajiriwa ili kujenga barabara, vituo vya askari wa wanyama pori, kuweka alama za mipaka, kutangaza na kusimamia miundombinu itakayowawezesha kuendesha miradi ya kijamii ya utalii yenye tija na iliyo endelevu. Sekta ya uzalishaji maua na mbogamboga (horticulture) nchini Tanzania, ambayo imeajiri zaidi ya wafanyakazi 10,000 na kuingiza zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 50 itasaidiwa kwa kupitia msaada utakaotolewa kwa Chama cha Wakulima wa Maua, Matunda na Mboga (TAHA) na wanachama wake ambao wengi wao ni wakulima wadogo wadogo wanawake. Aidha, msaada utatolewa kwa wafanyabiashara wanaouza mazao hayo nje ya nchi wanaohitaji mikopo ili kufufua na kuendeleza biashara zao na hivyo kuokoa ajira ya Watanzania.
Sera nzuri za fedha na uchumi ni kipengele muhimu cha uimara wa uchumi kwa kipindi kirefu.Msaada wa kukabiliana na athari za kuanguka kwa uchumi unaotolewa na watu wa Marekani utaisaidia Serikali ya Tanzania kufuatilia athari za kuporomoka kwa uchumi na kujenga msingi imara kwa kuhimili misukosuko ya kiuchumi katika siku zijazo. Kwa msaada kutoka Idara ya Misaada ya Kiufundi ya Wizara ya Fedha ya Marekani, Serikali ya Tanzania itaweza kuboresha mfumo wake wa upashanaji habari ili uwe na ufanisi na kuwezesha usimamizi wa fedha za umma wenye ufanisi na uwazi zaidi – hii ni pamoja na kuimarisha uwezo wa kufikisha kwa haraka zaidi rasilimali fedha katika maeneo yanayokabiliwa na upungufu wa chakula ambayo yametawanyika sana kijiografia.
Mbali na Mpango huu wa kubabiliana na athari za kuporomoka kwa uchumi duniani, USAID itashirikiana na mabenki ya hapa nchini katika kutoa mikopo yenye thamani ya hadi Dola za Kimarekani milioni 10 kwa ajili ya mitaji kwa shughuli za biashara inayohusisha kilimo na mazao ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kusaidia zaidi ya wazalishaji na wajasiriamali wadogo na kaya 1000 kwa kupitia taratibu za mikopo zenye masharti nafuu (micro-finance) katika kipindi cha miaka mitano ili kukuza uzalishaji na kuongeza uhakika wa chakula.
Ili kukuza manufaa ya ubia huu kwa uchumi wa Tanzania, angalau makampuni 50 ya Kitanzania yatahusishwa katika ununuzi na usambazaji wa chakula, usafirishaji na ubunifu na usimamizi wa uboreshaji wa miundombinu ya vijijini. Tanzania ni mojawapo kati ya nchi nane zitakazopatiwa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 255 chini ya mpango huu wa kukabiliana na athari za kuanguka kwa uchumi. Nchi nyingine za Kiafrika zitakazopatiwa msaada huu ni Ghana, Liberia na Zambia.




