Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Maonesho ya Vyuo Vikuu vya Marekani 2006

November 8, 2006

Ubalozi wa Marekani unawakaribisha wanafunzi wa shule za sekondari kuanzia kidato cha tatu na kuendelea, pamoja na wazazi wao, kuhudhuria Maonesho ya Vyuo Vikuu vya Marekani 2006 hapo Ijumaa tarehe 10 Novemba 2006. Maonesho hayo yatafanyika kwenye Ubalozi wa Marekani kuanzia saa 6:30 mchana mpaka saa 10:00 jioni.

Maonesho ya Vyuo Vikuu ya mwaka huu yanafanyika wakati wa maadhimisho ya saba ya kila mwaka ya Wiki ya Elimu ya Kimataifa (International Education Week), ambayo yanaandaliwa na Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje, ili kuenzi faida zinazotokana na kubadilishana kwa wanafunzi na waalimu kati ya Marekani na nchi zingine. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Elimu ya Kimataifa: Ushirikiano na Fursa za Maendeleo Ulimwenguni.” Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani, Maonesho ya Vyuo Vikuu yana lengo la kuwaelimisha watu kuhusu fursa za elimu ya juu kwa Watanzania zinazopatikana nchini Marekani. Lengo ni kuimarisha ubora na idadi ya wanafunzi wa Kitanzania wanaoomba kujiunga na vyuo nchini Marekani.

Waziri wa Elimu wa Marekani, Margaret Spelling alisema, “Mambo yote yanaanzia na elimu bora, na elimu ni maadili yanayotuunganisha pamoja ulimwenguni kote, na pia ni msingi wa mustakabali mzuri kwa watoto wetu. Zaidi ya yote, mafanikio katika ulimwengu wa leo yanategemea mambo unayoyafahamu, na siyo sehemu unayoishi. Teknolojia imesawazisha uwanja wa fursa na ‘kuushusha’ ulimwengu chini. Pia imeonyesha thamani ya hesabu, sayansi na masomo mengine yanayopendwa na watu wengi duniani kote,” alisema.

Washiriki kwenye maonesho hayo watapewa taarifa kuhusu mchakato wa wanafunzi kupata visa ya kuingia Marekani, na pia wataelimishwa kuhusu madhumuni na faida za Maonesho ya Vyuo Vikuu.

Mada zingine ni pamoja na: mfumo wa elimu ya juu, jinsi ya kugharamia elimu ya juu kwa wanafunzi wanaotoka nje ya Marekani, pamoja na mchakato wa kujiunga na vyuo vikuu vya Marekani. Washiriki kwenye maonesho hayo watapata fursa ya kufahamishwa kuhusu maisha ya chuo kikuu nchini Marekani na maafisa wanaoandikisha wanafunzi kutoka Baraza la Shule za Kimataifa - Council for International Schools (CIS), pamoja na wanafunzi wa zamani wa vyuo hivyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya 2005 ya taasisi inayoshughulikia elimu ya kimataifa - Institute for International Education’s Annual Open Doors, Tanzania inachukua nafasi ya saba barani Afrika kwa idadi ya wanafunzi wanaosoma Marekani, baada ya Kenya, Nigeria, Ghana, South Africa, Zimbabwe na Cameroon.

- Translation -
This content is also available in English