| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari
Serikali ya Marekani yatoa mafunzo ya teknolojia ya kuchunguza makosa ya jinai kwa Jeshi la Polisi Tanzania
Novemba 9, 2006
Serikali ya Marekani inatoa mafunzo ya kiufundi na wataalamu kwa Jeshi la Polisi kama juhudi za matayarisho kabla ya kufunguliwa kwa Kitengo cha Kemia cha Maabara ya Kuchunguza Makosa ya Jinai cha Jeshi la Polisi Tanzania. Serikali ya Tanzania imekarabati eneo lote la ghorofa ya pili ya jengo la Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar-es-Salaam. Eneo hilo lenye ukubwa wa futi 18,600 mraba litakuwa ni maabara ya kisasa ya kuchunguza makosa ja jinai, baada ya vitengo vinavyoshughulikia uchunguzi wa sumu (toxicology), dalili na alama (trace), na baiolojia kumalizika.
Mwanasayansi mashuhuri wa uchunguzi wa makosa ya jinai na mwandishi wa vitabu vya fani hiyo, Terry Mills, ataendesha kozi ya wiki mbili nchini Tanzania kuwafundisha wanakemia wa Jeshi la Polisi somo la Misingi ya Kemia ya Kuchunguza Makosa ya Jinai (Basic Forensic Chemistry). Kozi hiyo itahusisha marudio ya misingi ya kemia na italenga zaidi kutoa ujuzi wa kemia unaohitajika kupima ushahidi katika kuchunguza makosa ya jinai. Mpango wa kimataifa wa Wizara ya Sheria ya Marekani wa kutoa mafunzo ya uchunguzi wa makosa ya jinai (United States Department of Justice/International Criminal Investigative Training Program) umekuwa ukitoa mafunzo kama haya kwa Tanzania kwa muda wa miaka minne iliyopita.
Bi. Carla Noziglia, mshauri mwandamizi wa sayansi ya kuchunguza makosa ya jinai (senior forensic advisor) wa Serikali ya Marekani amekuwa akiratibu shughuli za kutoa mafunzo na kuweka mitambo kwenye maabara hiyo iliyogharimu sh. bilioni 3.2. Serikali ya Marekani imetoa msaada huo kupitia kitengo cha kudhibiti mihadarati cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani. (U.S. Department of State’s Bureau of International Narcotics and Law Enforcement - INL).



