| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Balozi wa Marekani Aungana na TACAIDS Kuadhimisha SIku ya Ukimwi Duniani
Desemba 1, 2005Songea, Dec 1, 2005 – Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Retzer, ameshiriki katika kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani iliyoandaliwa kitaifa na TACAIDS mjini Songea, ambapo amegusia umuhimu wa upimiaji wa hiari ili kufanikisha kuwagundua wale ambao wanahitaji matibabu ya ugonjwa huo.
Balozi Retzer ameeleza kwamba bila kinga ya Ukimwi, kutakuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu watakaohitaji matibabu. Upimaji wa hiari ndio njia pekee ya uhakika ya kuweza kugundua wale walioko hatarini na wanaweza kujikinga kutokana na ushauri watakoupata; hali kadhalika wale watakaohitaji matibabu kutokana na ugonjwa. Kwa maana hiyo, alisema Balozi Retzer, upimaji wa Ukimwi ni hatua moja muhimu sana kwa ajili ya kufanikisha programu ya TACAIDS.
Karibu kote barani Africa, upimaji wa Ukimwi umekuwa wa kiwango cha chini kwa asilimia 10 tu ikilinganishwa na hali halisi ya watu walioko hatarini. Hata sehemu ambazo upimaji unapatikana kirahisi, idadi ya watu wanaojinufaisha na huduma hiyo bado ni ndogo sana. Kuachana na unyanyapaa katika upimaji na kujenga mazingira ya kuweza kujadili kuhusu ugonjwa huo ni muhimu, endapo tunataka kufanikiwa kukabiliana na kirusi hiki.
Balozi huyo ambaye alikuwa ameambatana na wakurugenzi wa Timu ya Mpango wa Dharura wa Marekani (Stephan Wiktor – Mkurugrnzi wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC); Pamela White - Mkurugenzi wa USAID, Christine Djondo – Mkurugenzi wa Peace Corps na Luteni Kanali Laura Varhola – Kitengo cha Ulinzi), alitumia tukio hilo kuelezea alichokiita ‘The 3 Cs’ “Upimaji wa mtu mmoja mmoja lazima uwe wa siri (confidential), ni lazima iambatane na ushauri nasaha (counseling), na inaweza kufanyika tu kwa mtu mpimwaji mwenyewe kukubaliana nayo (consent), ikimaanisha kwamba ni suala lililo wazi la hiari,” alisema.
Serikali ya Marekani imesaidia kutoa ushauri nasaha na upimaji wa hiari kwa karibu robo milioni ya Watanzania kwa mwaka uliopita pekee. Lakini licha ya namba hiyo kuonekana kubwa – ukichukulia kwamba mmoja kati ya Watanzania 15 anahisiwa kuwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi – idadi ya watu waliojitolea kupimwa mwaka jana ni moja ya kumi ya idadi ya wale wanaoweza kuwa wameambukizwa na ugonjwa huo.
Kutokana na hilo, Mpango Maalum wa Rais wa Marekani wa Kupunguza Makali ya Ukimwi (PEPFAR) unalenga pia katika kujenga miundo mbinu na uwezo wa kibinadamu wa kugundua na kutibu madhara yanayosababishwa na ugonjwa huo. Mwaka uliopita, serikali ya Marekani imeongeza idadi ya vipeperushi vinavyopasha kuhusu upimaji na ushauri nasaha, wakati huohuo, kuongeza idadi ya watu waliofunzwa kusimamia upimaji wa Virusi Vya Ukimwi. Huduma hizi muhimu zimepangwa kuongezeka maradufu katika miezi na miaka ijayo.



