Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Serikali ya Marekani yatoa msaada wa jenereta na vyandarua kwa maabara ya afya Pemba

Desemba 19, 2005

Sambamba na uzinduzi wa mpango wa Rais wa Marekani wa kupambana na ugonjwa wa malaria (U.S. President’s Malaria Initiative - PMI) nchini, na kama hatua ya kudhihirisha juhudi za Marekani kuisaidia Zanzibar, Kaimu Balozi wa Marekani Daniel Purnell Delly anaenda Pemba leo akifuatana na maafisa wa shirika la misaada la USAID kukabidhi misaada ya jenereta na vyandarua 200 vilivyotiwa dawa ya kuua mbu. Baadaye, Bwana Delly na maafisa wengine wa Marekani wataenda Unguja kusherekea uzinduzi wa mpango wa kudhibiti malaria visiwani Zanzibar, ‘Kataa Malaria.’ Mpango huu unafadhiliwa na shirika la misaada la USAID, vituo vya Marekani vya kudhibiti maradhi vya CDC (U.S. Centers for Disease Control), pamoja na mfuko wa Global Fund.

Mpango wa Rais wa Marekani wa kupambana na malaria ambao utaleta misaada ya dola milioni 11.5 nchini Tanzania kwa mwaka wa 2005/2006 (zikiwemo dola milioni 3 kwa Zanzibar), unafanya juhudi kupunguza kwa nusu idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa malaria nchini Tanzania. Akina mama waja wazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ndio hasa watakuwa walengwa wa mpango huu, zikiwemo mbinu mbalimbali za kinga - - matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuua mbu, kupulizia dawa ndani ya nyumba, tiba ya kuzuia malaria wakati wa uja uzito, na kutolewa kwa dawa madhubuti ya Artemisinin ya kutibu malaria.

Kuadhimisha uzinduzi huu, shirika la USAID litatoa misaada ya takriban vyandarua 200 vilivyotiwa dawa kwa asasi kadhaa zisizo za Serikali zinazoshughulikia watoto yatima, watoto wanaoishi katika mazingira magumu, pamoja na watu wanaoishi na UKIMWI. Asasi zitakazonufaika na misaada hiyo ni pamoja na Pemba Island Relief Organization (PIRO) na mfuko wa watoto wa Zanzibar, Children’s Fund (ZCF). Watoto yatima na watu wanaoishi na UKIMWI ni makundi ya watu wanaoambukizwa malaria kwa urahisi sana. Vyandarua hivi vitasaidia kupunguza maambukizi ya malaria miongoni mwa makundi yaliyotajwa huko Pemba. Vyandarua vingine vilivyotiwa dawa vitafuata hivi karibuni kwa ajili ya watoto walio chini ya miaka mitano na akina mama waja wazito, kama sehemu ya mpango wa Rais wa kupambana na malaria.

Akiwa Pemba, Kaimu Balozi wa Marekani pia atakabidhi kwa kitengo cha maabara ya afya ya jamii jenereta aina ya Perkins yenye thamani ya dola 14,000 ambayo ina uwezo wa KVA 40. Umeme wa kuaminika ni muhimu sana katika kutoa huduma nzuri za maabara, hasa katika enzi hizi za kutumia kompyuta katika kuendesha shughuli za maabara. Maabara hiyo ina jukumu muhimu katika kufanikisha vita dhidi ya maradhi kisiwani Pemba. Upatikanaji wa umeme unaoaminika utawezesha vipimo na shughuli mbalimbali za maabara kufanyika kwa ufanisi hata kama umeme wa kawaida utakatika.

- Translation -
This content is also available in English