| - Translation - |
| This content is also available in English |
Taarifa kwa vyombo vya habari
Afisa mwandamizi wa Marekani atembelea Pemba, afungua jumba la makumbusho
Desemba 22, 2005
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Dr. Jendayi Frazer, pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman leo walifungua rasmi Jumba la Makumbusho la Pemba, mjini Chake Chake. Mfuko wa Balozi wa Kuhifadhi Utamaduni ulio chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani (U.S. Department of State’s Ambassador’s Fund for Cultural Preservation), ambao lengo lake ni kusaidia miradi ya kuhifadhi utamaduni duniani kote, ulichangia kukarabati jumba hilo la makumbusho.
Mradi wa kukarabati jumba hilo ulifadhiliwa kupitia msaada wa zaidi ya Sh. milioni 27 uliotolewa kwa Idara ya Nyaraka, Makumbusho na Mambo ya Kale kufanya ukarabati mdogo wa jengo hilo na shughuli mbalimbali. Naibu Waziri Frazer alisema kuwa amefurahi sana kushiriki katika ufunguzi huo, na kumpongeza Dkt. Hamad Omar na wafanyakazi wa Idara ya Nyaraka, Makumbusho na Mambo ya Kale kwa kazi nzuri wanayoifanya. “Kisiwa hiki kina historia ndefu,” aliwaambia wageni waalikwa, “na ni muhimu kwamba historia hii ihifadhiwe kwa matumizi yenu, watoto wenu na vizazi vijazo. Jumba la Makumbusho litafanikisha azma hii.”
Jumba la Makumbusho la Pemba ni sehemu ya kuhifadhia urithi wa utamaduni wa Pemba. Hapo nyuma hapakuwa na sehemu kama hiyo kisiwani humo. Maonyesho kwenye jumba hilo yanawawezesha wananchi na watalii wengi wanaokitembelea kisiwa hicho kujifunza historia ndefu ya Pemba. Jumba hilo linaonyesha historia ya Pemba kuanzia karne ya tano mpaka leo. Makumbusho yamegawanyika katika vitengo vitano: Historia ya kale ya Pemba, historia ya ubaharia, jamii mbalimbali, jela (inaamika hii ilikuwa mahabusu ya askari wa Kireno waliokosa nidhamu), na nyumba ya Kiswahili. Mradi huu pia umefanikisha kuhifadhiwa kwa nyaraka adimu za kale, na umetoa nafasi kwa wanafunzi kukusanyika hapo kwa shughuli za kishule.
Pamoja na kuzindua Jumba la Makumbusho la Pemba, Naibu Waziri Frazer pia alifanya mazungumzo na viongozi wa Kiislamu kisiwani humo ambayo yalikuwa yameaandaliwa na Ofisi ya Mufti. Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Naibu Waziri wa Marekani au mtu mwingine mwenye hadhi kama hiyo kukitembelea kisiwa hicho.
Dkt. Frazer aliwasili nchini mwanzoni mwa wiki hii kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Kikwete. Baadaye alifanya mazungumzo na Rais pamoja na maafisa wengine wa Tanzania pamoja na wawakilishi wa vikundi vya jamii raia, kujadili masuala mbalimbali yanayozihusu nchi hizi mbili. Aidha, akiwa jijini Dar-es-Salaam, Naibu Waziri alitoa mada kwenye Chuo cha Diplomasia juu ya “Uhusiano kati ya Marekani na Tanzania mwanzoni wa utawala wa Rais Kikwete.”



