Speeches
Sherehe ya kukabidhi hundi za Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi Midogo Midogo
Mahali: Ubalozi wa Marekani
Februari 1, 2008
Hotuba ya Balozi Mark Green (kama ilivyotayarishwa)
Ni furaha yangu kuwakaribisheni ninyi wote hapa asubuhi ya leo kutangaza vikundi vitakavyopokea misaada kutoka kwa moja ya mipango muhimu sana ya Ubalozi wa Marekani – Mfuko Maalum wa Balozi wa Kusaidia Miradi Midogo Midogo (Ambassador’s Special Self-Help Fund).
Mara kwa mara watu huniuliza, “Marekani inawakilisha nini? Hivi Wamarekani wanaamini katika kitu gani, kupita kitu chochote?”
Jawabu ni rahisi sana: Tunaamini katika fursa. Tunaamini katika kuwasaidia wananchi wa kawaida kupata fursa ya kubadili maisha yao na yale ya jamii zao.
Hii ndiyo maana halisi ya sherehe ya leo. Misaada hii inalenga kusaidia jamii kwenye ngazi ya kijiji. Kwa sababu – kama mnavyofahamu – mabadiliko halisi daima huanzia kwenye ngazi ya kijiji.
Misaada hii ni jawabu la Ubalozi kwa maombi ya kusaidia miradi midogo midogo ya jamii nchini kote Tanzania. Mfuko Maalum wa Balozi wa Kusaidia Miradi Midogo Midogo unajivunia historia ndefu ya ushirikiano na jumuia za Watanzania, tangu mwaka wa 1965.
Kutoka Tunduru mpaka Zanzibar, kutoka Karagwe mpaka Tarime, misaada hii ya kuwawezesha wananchi wajisaidie wenyewe, imechangia kuboresha huduma za usafi, elimu, maendeleo ya kiuchumi, pamoja na mifumo ya kuvuna maji. Mfuko huu unadhihirisha nia njema na juhudi za dhati za wananchi wa Marekani katika kusaidia maendeleo kwenye jumuia, pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wa Tanzania.
Katika nusu ya pili ya mwaka wa 2007, Mfuko Maalum wa Balozi wa Kusaidia Miradi Midogo Midogo uliidhinisha jumla ya misaada 16 yenye thamani za dola 70,000, ili kusaidia kuanzishwa kwa miradi mipya nchini Tanzania. Misaada hii itafadhili miradi ya huduma za jamii, maji na usafi, na kwenye sekta ya misaada ya kijamii.
Kila kikundi kimevumilia mchakato mrefu wa maombi uliodumu takriban mwaka mmoja – na wanastahili kutambuliwa kimaalum kwa kukamilisha mchakato huo, ili waweze kuwa hapa leo kupokea hundi zao na kutia saini mikataba ya misaada hiyo.
Miongoni mwa vikundi vitakavyopewa misaada hiyo mwaka huu ni pamoja na shule huko Zanzibar, chama cha ushirika cha washonaji huko Njombe, na mifumo ya kuboresha huduma za maji huko Karagwe, Shinyanga na wilayani Temeke hapa Dar es Salaam.
Kila mradi utachangia kwa kiasi kikubwa kufungua fursa za kiuchumi, kuhamasisha maendeleo, pamoja na kujenga mustakabali mzuri kwa Watanzania kwenye ngazi ya kijiji. Hakuna shaka, umuhimu wa mfuko huu maalum ni kwamba, huu ni msaada wa kutoka kwa wananchi kwenda kwa wananchi; kutoka kwa wananchi wa Marekani kwenda kwa wananchi wa Tanzania.
Huko nyumbani kwetu katika Jimbo la Wisconsin, watu wengi wanaishi kwenye vijiji vidogo vidogo. Kusema kweli, mke wangu Sue ambaye yuko nasi hapa leo, alikulia kwenye jumuia ndogo ya wakulima huko Wisconsin. Wananchi hawa wa Marekani wanakabiliwa na kuelewa matatizo mengi, kama yale wanayoyapata wananchi wa Tanzania katika vijiji vyenu, kuhusiana na upatikanaji wa huduma muhimu.
Lakini Wamarekani hawa wanatambua pia kwamba, wanatoka kwenye nchi yenye baraka, na wanajua kuwa wana wajibu wa kuwagawia wananchi wa Tanzania baadhi ya baraka hizo. Ingawa msaada unaotolewa na mfuko huu ni chini ya shilingi milioni sita kwa wastani, tuna imani kuwa mtaitumia misaada hii ambayo ni kama mbegu, vizuri na kwa ufanisi, ili kuboresha miradi muhimu kwenye jumuia zenu.
Tuna imani nanyi, na tuna imani na mustakabali wenu. Hii ndiyo maana tunasimama pamoja nanyi, na tunapenda kuwasaidia kufanikisha mipango yenu.
Kwa mara nyingine tena, nachukua fursa hii kupongeza kila moja ya vikundi 16 vinavyopewa misaada hii. Ninajua kuwa mameneja wa miradi waliopo hapa leo wanawakilisha matumaini ya vijiji katika kila kona ya Tanzania.
Timu yangu inasubiri kwa hamu kuona ripoti za maendeleo, kuhusu jinsi miradi yenu inavyoendelea. Na miradi yenu itakapokamilika, watu kutoka kwenye timu yangu watakuwa na shauku kutembelea miji yenu kuhudhuria sherehe za uzinduzi.
Hongera kwenu wote, na ninawatakia kila la kheri katika kazi zenu!
Asanteni sana



