Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Hotuba na Kaimu Naibu Balozi, Dk. Tulinabo Mushingi kwenye Uzinduzi wa Miskiti Micheweni
Skip Left Section Navigation

Speeches

Uzinduzi wa Miskiti Micheweni

Pemba, Zanzibar

Machi 9, 2009

Hotuba na Kaimu Naibu Balozi, Dk. Tulinabo Mushingi

Asalam Alaykum
Waheshimiwa wageni Waalikwa
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ndugu Khamis Jabir Makame
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Ndugu, Dadi Faki Dadi
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Pemba Kusini, Ndugu Kassim Juma Tindwa
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Ndugu, Ali Adballah Juma
Masheikh, Masheha, Mabibi na Mabwana:

  • Ni heshima kubwa na ya kipekee kuungana nanyi hivi leo katika kusherehekea kukamilika kwa ukarabati wa misikiti katika shehia za Micheweni na Shumba. Ukarabati wa misikiti hii ya kihistoria ni hatua kubwa. Kazi hii muhimu imewezekana kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya watu wa Marekani na wananchi wa Tanzania na inaashiria ubia imara uliopo baina ya nchi zetu mbili.


  • Idara ya Mambo ya Kale ya Zanzibar ilibainisha haja na umuhimu wa kukarabati misikiti hii ya kipekee na ya kihistoria na kutujulisha kuhusu jambo hilo. Marekani na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi zinazothamini na kuheshimu sana tofauti za kiimani katika jamii zetu. Kwa sababu hiyo tulipofahamu kuwa misikiti hii muhimu ya kihistoria na kitamaduni ilikuwa ikihitaji ukarabati, tulikuwa tayari kusaidia.


  • Kwa kupitia mfuko wa Ubalozi wa Marekani wa Kusaidia Shughuli za Kiutamaduni, tuliweza kutoa zaidi ya Dola 25,000 (sawa na zaidi ya Shilingi za Kitanzania 32 Milioni) kwa shehia zenu mbili kwa ajili ya ukarabati wa miskiti hiyo.


  • Aidha, tunafurahi kwamba kwa sehemu kubwa kazi ya usimamizi na ukarabati ilifanywa na ninyi wenyewe. Kwa miaka kadhaa, kazi hiyo imefanywa kwa uhodari na umakini mkubwa. Mitindo na nakshi za kipekee za misikiti hii, zinazojumuisha tamaduni za ujenzi za Kiswahili na Kiajemi za kuanzia karne ya 17 na 18, zimehifadhiwa vyema na zitatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo vya Micheweni na Shumba.


  • Nafikiri nyote mtakubaliana nami kuwa misikiti hii miwili ya kihistoria imekarabatiwa vizuri sana kwa ajili ya watu wote wanaofanya ibada katika shehia hizo.


  • Kukamilika kwa miradi hii muhimu ni kieleleza cha ubia wa dhati baina ya Serikali zetu mbili, na tunaamini kuwa tutaendelea kusherehekea pamoja nanyi kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa miaka kadhaa iliyopita.


  • Ninapenda pia kuchukua fursa hii, kuwasilisha salamu zetu za rambirambi kufuatia kifo cha Sheikh Kombo Rashid. Alikuwa kiongozi mzuri wa jamii hizi. Mara zote alitukaribisha vizuri na kwa ukarimu mkubwa tulipotembelea shehia hizi na wakati wote alitupa ushirikiano mkubwa. Tunatambua kuwa alikuwa ni nguzo muhimu na mtu aliyetoa msukumo mkubwa katika kukamilisha sehemu ya mradi huu wa ukarabati. Aidha tunatambua kuwa ameacha pengo kubwa.


  • Kwa kumalizia, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati kwa kunipa fursa hii ya kushiriki nanyi katika uzinduzi wa misikiti hii hivi leo. Najisikia fahari kubwa kuiwakilisha Serikali ya Marekani na kupongeza mchango wa watu wa Marekani katika kuboresha hali ya maisha ya jamii hizi. Kwa niaba ya Watu wa Marekani, napenda kuwapongeza kwa dhati wananchi wa shehia za Micheweni na Shumba. Ninatoa wito na kuwahimiza watoto wa shehia hizi kusoma kwa bidii. Hakika mustakabali wenu utakuwa mwema zaidi!

Asenteni sana!