Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Hotuba ya Mwakilishi wa CJTF – HOA Kwenye Uzinduzi Wa Mradi Wa Maji – Urambo
Skip Left Section Navigation

Speeches

Uzinduzi Wa Mradi Wa Maji – Urambo

Machi 11, 2009

Hotuba ya Mwakilishi wa CJTF – HOA

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa:
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya:
Waheshimiwa Wenyeviti wa Vijiji:
Waheshimiwa Wazee wa Kijiji :
Mheshimiwa Diwani:
Mheshimiwa Mbunge:
Mabibi na Mabwana:

Kwa niaba ya Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kanda ya Pembe ya Afrika, Kamanda Tony Kurta, ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa viongozi, wananchi wa Urambo na mafundi wa uchimbaji visima kwa kazi kubwa mliyoifanya.

- ASANTENI!

Ni heshima kubwa sana kwangu kuwa hapa leo, tukiadhimisha ubia na ushirikiano kati ya Kikosi Maalumu cha Pembe ya Afrika na watu wa Tanzania, hususan wa Mkoa wa Tabora.

Maji ni uhai. Hivyo ni jambo jema sana kwamba ushirikiano wenu, wa viongozi wenu, wa serikali yenu na wa serikali ya Marekani, umewezesha mradi huu mzuri wa maji kutekelezwa. Kwa pamoja tumewezesha kupatikana kwa visima vya maji 17 zaidi katika mkoa huu. Mafanikio haya ni mfano mzuri wa yale yanayoweza kufanyika pale ambapo watu, jamii na nchi zinaposhirikiana. Tunathamini sana ushirikiano mzuri uliopo baina yetu na kwamba matokeo ya ubia wetu imara ni kuimarika kwa utulivu wa kikanda na panapokuwa na utulivu, migogoro na migongano katika jamii hupungua. Ninatoa pengezi zangu za dhati kwa mafundi wachimbaji wa visima kwa jitihada kubwa na kujitoa kwao kwa dhati katika utekelezaji wa mradi huu na katika kushughulikia vyema changamoto nyingi zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake kwa kuwa na mawasiliano ya wazi nanyi. Jambo hili limeimarisha uhusiano wetu na Tanzania hasa tunapotaka kujenga mahusiano mema katika kanda yote. Tunawashukuru sana kwa maelewano, ushirikiano na ukarimu wenu.

Leo hii tunakabidhi visima hivi vya maji kwa jamii ya watu wa Urambo. Visima hivi ni vyenu na vya jamii nzima kwani vitakuwa vikitoa maji safi kwa familia na mifugo yenu. Wito wetu ni kwamba, vitunzeni vizuri ili viendelee kufanya kazi na kuwahudumia kwa miaka mingi ijayo.

Mwisho, Kikosi maalumu cha Kanda ya Pembe ya Afrika na Serikali ya Marekani inalenga katika kuwasaidia Waafrika kujiletea utulivu na usalama. Mradi huu wa maji ni kielelezo kimojawapo cha azma yetu ya kusaidia Afrika kuwa salama, imara na tulivu.

Kwa mara nyingine tena, tunatoa shukrani kwa heshima hii kubwa ya kuwa sehemu ya sherehe hizi za uzinduzi wa visima. Tunatarajia kuwa urafiki baina yetu na watu wa Urambo na nchi nzima ya Tanzania utaimarika na kudumu.

ASANTENI.