Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Hotuba na Kaimu Balozi wa Marekani Larry André kwenye Uzinduzi wa Kitabu: Programu ya Elimu ya Awali ya Madrasa
Skip Left Section Navigation

Speeches

Uzinduzi wa Kitabu: Programu ya Elimu ya Awali ya Madrasa

Dar es Salaam, Tanzania

Aprili 2, 2009

Hotuba na Kaimu Balozi wa Marekani Larry André (kama ilivyotayarishwa)

Waheshimiwa wageni waalikwa,
Rais Karume na waheshimiwa wawakilishi wa Serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano,
Wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Aga Khan
Wawakilishi wa Ummah
Rais Kikwete, Oyee!
Rais Obama, Oyee!
Mabibi na mabwana, habari za asubuhi!
Asalam Alaykum!

Nina furaha kubwa kujumuika nanyi hivi leo katika hafla hii ya uzinduzi wa kitabu kinachoelezea kazi na rekodi nzuri ya mafanikio ya Programu ya Elimu ya Awali ya Madrasa katika kipindi cha zaidi ya miaka 25 iliyopita.

Kama ilivyo kwa wazazi wengi wa Kitanzania, Rais Obama anaamini kuwa uwekezaji katika elimu ya watoto wetu ni uwekezaji katika mustakabala wa nchi yetu. Maamuzi yanayofanywa na viongozi wetu kuhusu elimu ndiyo yanayoamua hali ya baadaye ya vizazi vijavyo vya taifa. Elimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kisiasa. Ukuaji wa uchumi unahitaji nguvu kazi iliyoelimika vyema. Aidha, demokrasia hushamiri pale ambapo raia wana elimu na ujuzi wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu sera na viongozi wanaotafuta kuungwa mkono na wananchi. Kama ilivyo kwa Programu ya Elimu ya Awali ya Madrasa, huko nyumbani Marekani, Rais Obama anatekeleza Mpango wa Elimu na Makuzi ya Awali ya Watoto toka Wanapozaliwa hadi Miaka Mitano (Early Childhood Education Zero to Five Plan) ili kutoa misaada unaohitajika kwa watoto hao na wazazi wao.

Ninajivunia sana ubia wetu na Serikali ya Tanzania na Taasisi ya Aga Khan. Serikali ya Marekani na Shirika la Maendeleo la Aga Khan tumekuwa na historia ya muda mrefu ya kufanya kazi kwa ubia katika nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Pakistan, Afghanistan, India, na Mali. Ubia wetu katika kanda hii unalenga zaidi katika suala la elimu. Sote tuna dhamira ya dhati ya kuisaidia Tanzania ili watoto wake wote, bila kujali hali zao za ulemavu, umasikini, jinsia au hata maradhi. Mradi wetu mkubwa zaidi ni ule wa kuwasaidia watoto wa Kitanzania kupata fursa ya kwenda shule, kuendelea na masomo na hatimaye kumaliza shule (the Completion, Retention and Access for Tanzanians to Education – CREATE) ulioanza mwaka 2007. Mradi huu unaendesha shughuli zake zaidi huko Zanzibar na katika mikoa ya pwani ya kusini mwa Tanzania bara, yaani Mtwara na Lindi. Mradi wa CREATE unalenga katika kufikia matokeo makuu matatu: kuinua ubora wa fursa za elimu ya awali na elimu ya msingi kwa watoto kutoka katika jamii masikini; kuinua kiwango cha uelewa na kufaulu kwa wanafunzi wa shule za sekondari katika masomo ya Hisabati na Sayansi; na kuimarisha mikakati ya serikali ya kuinua sekta ya elimu. Mradi huu wa miaka mitatu unatekelezwa kwa ufadhili wa na Watu wa Marekani na Taasisi ya Aga Khan wa zaidi ya Dola milioni 5. Aidha, mradi unaendeshwa kwa ubia na Wizara zinazoshughulikia elimu katika Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.

Ninapenda kutambua na kupongeza mchango mkubwa wa uongozi wa jumuiya ya Waislamu Tanzania, Mufti Mkuu, Kadhi Mkuu na BAKWATA. Mwongozo wao ndio ulioiwezesha programu hii ya shule tunayoifadhili iweze kukidhi utamaduni,amali na maadili ya kiroho ya jumuiya ya Waislamu wa Tanzania. Waislamu wametoa mchango mkubwa katika ustaarabu wa dunia katika sanaa na sayansi. Msaada ambao mradi huu unaupata kutoka kwa viongozi wakuu na Ummah wa Waislamu unaendeleza utamaduni huo wa kujivunia.

Kituo cha Mafunzo na Maktaba Kuhusu Madrasa cha Zanzibar kimekuwa ni mshirika muhimu katika mradi wa CREATE. Kwa msaada wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) na Taasisi ya Aga Khan, kituo hiki kimeweza kupanua shughuli zake visiwani Zanzibar na kuanza kufanya kazi na shule za awali katika mikoa ya Mtwara na Lindi, na kwa hali hiyo kuleta utaalamu na uzoefu wa kutoka Zanzibar Tanzania bara.

Tunafurahi sana kwamba kitabu hiki kinatoa ushahidi wa wazi kabisa wa umuhimu wa kuhakikisha makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto katika hatua za awali kabisa za maisha yake. Utafiti unaonyesha kuwa watoto wa Kitanzania ambao wamepata fursa ya elimu bora ya awali wana nafasi kubwa zaidi kufanya vizuri na kuendelea na masomo yao shuleni kuliko wale ambao hawakupata fursa hiyo. Tafiti zilizofanyika nchini mwangu zinabaisha hali hiyo hiyo.

Tunashukuru sana kwa heshima tuliyopewa na wabia wetu wa Kitanzania katika kutuomba tufanye kazi pamoja katika kusaidia elimu. Huu ni wajibu muhimu sana, kwa kuwa sote tunaelewa kuwa watoto wa Kitanzania ndio watakaokuwa viongozi wa taifa hili katika siku zijazo.

Asanteni sana!