Skip Navigation
Skip Left Section Navigation

Speeches

Hotuba fupi ya Balozi Michael L. Retzer Sherehe ya kuadhimisha kukamilika kwa mradi uliofadhiliwa na fuko wa Balozi wa Kuhifadhi Utamaduni: Kuhifadhi na kusambaza nyaraka na vitu vinavyohusiana na biashara ya utumwa, kwenye Idara ya Nyaraka, na Mambo ya Kale, Zanzibar

Venue: Jumba la Wananchi, Zanzibar. April 27, 2006

Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni na Mafunzo ya Amali;
Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho, Nyaraka, na Mambo ya Kale;
Wageni Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;

  • Asalaam Alaykum! Asanteni sana kwa kuhudhuria sherehe hii ya leo. Ni matumaini yangu kwamba mtafurahia kuwa nasi, na kwamba kama mimi, mtajifunza mambo machache kuhusu historia ya biashara ya utumwa katika eneo la Bahari ya Hindi.

  • Tumewakaribisheni hapa leo kuadhimisha kukamilika kwa mradi muhimu sana wa kuhifadhi urithi wa utamaduni wa watu wa nchi hii. Kupitia msaada wa kifedha uliotolewa na Serikali ya Marekani, Wizara yenu imefanikiwa kukarabati, kuhifadhi, kuingiza kwenye katalogi, na kuchapisha baadhi ya nyaraka muhimu duniani za kihistoria, zinazohusiana na biashara ya utumwa katika eneo la Bahari ya Hindi. Haya ni mafanikio makubwa na ninafikiri kwamba wote waliohusika wanastahili pongezi.

  • Nyaraka hizi zinaonyesha unyama wa biashara ya utumwa kupitia sauti za watu waliokuwa wakiishi wakati huo. Kwa kufanya hivyo, wametusaidia sisi wote kuelewa jinsi ya kuzuia vitendo kama hivyo visitokee tena katika siku za mbele.

  • Kitu kingine ambacho nyaraka hizi zinafanya, ni kutupa sisi mwanga wa kuielewa historia inayovutia ya Visiwa vya Zanzibar. Nilikuwa nikisoma kijitabu cha kumbukumbu za watumwa Zanzibar, ambacho kimechapishwa kama sehemu ya mradi huu. Hadithi zake ni za kusisimua kweli. Kwa mfano, kuhusu mapambano kati ya Waingereza waliokuwa wakishinikiza kukomeshwa kwa utumwa, na Sultan wa Oman ambaye alikuwa akipinga hatua hiyo. Mapambano haya yameelezwa kwa kina katika kijitabu hicho. Kama bado hamjakisoma, basi ninawashauri mfanye hivyo.

  • Lakini jambo kubwa zaidi lililofanikishwa na mradi huu ni kuhifadhi sehemu muhimu ya utamaduni wa Zanzibar. Biashara ya utumwa siyo tu kwamba ni simulizi za kusisimua kwa wananchi wa visiwa hivi. Biashara hii ndiyo sababu kwa nini wengi wa mababu zenu walikuja hapa; pia ndiyo iliyoweka mpangilio wa makazi, mifumo ya kiuchumi na kisiasa; na pia ilibainisha aina ya muziki, ngoma na nyimbo za wananchi vijijini, pamoja na desturi za kidini. Kwa kifupi, biashara ya utumwa iligusa kwa kina kila sehemu ya maisha katika visiwa hivi. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwamba muendelee kuziweka hai nyaraka hizi pamoja na vitu vingine ambavyo vinaelezea hadithi hii.

  • Hii ndiyo sababu kwa nini Serikali yangu ilitoa msaada kufanikisha mradi huu. Tunaelewa umuhimu wa historia, mila na utamaduni, kwa wananchi wa Zanzibar, na tungependa kuendelea kuwasaidieni kuienzi historia yenu. Kama Wamarekani, tunalichukulia suala la kuhifadhi utamaduni kwa makini sana. Kama Bwana Omar, Mkurugenzi wa Idara ya Nyaraka na Mambo ya Kale, anavyoweza kuwathibitishieni, baada ya kufanya ziara ya kutembelea nyumba zetu za makumbusho nchini Marekani mwaka jana. Tunalipa suala hili la kuhifadhi utamaduni umakini mkubwa.

  • Kwa sababu hiyo, Serikali yangu ilianzisha mfuko wa Balozi wa kusaidia shughuli za kuhifadhi utamaduni mwaka wa 2001, ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kuhifadhi urithi wa utamaduni wao, na kudhihirisha kwamba tunaheshimu tamaduni zingine. Tunaruhusiwa kufadhili mradi mmoja tu katika kila nchi iliyochaguliwa. Huu ni mchakato wenye ushindani mkubwa. Mapendekezo ya miradi kutoka Ubalozi wetu yanashindana na yale yaliyowasilishwa na balozi zingine duniani kote. Ninafurahi kusema kwamba katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Tanzania imeweza kupata ufadhili katika miaka mitatu.

  • Kupitia mfuko huu, tumeweza kusaidia kuhifadhi mziki wa jadi kwa kushirikiana na chuo cha mziki cha nchi zinaotumia madau - Dhow Countries Music Academy; tumefadhili ujenzi wa makumbusho ya Pemba; na sasa hivi tumesaidia kuhifadhi na kusambaza taarifa kuhusu biashara ya utumwa. Tunaendelea kushughulikia miradi ya hapo baadaye, ambayo nina uhakika itaendeleza rekodi hii nzuri ya mafanikio.

  • Inawezekana baadhi yenu mnajiuliza: Kwa nini Serikali ya Marekani inatumia pesa nyingi katika miradi ya kuhifadhi utamaduni, wakati kuna umaskini mkubwa Visiwani Zanzibar? Ningependa kuwaambieni kuwa, utamaduni wenu ni moja ya nguvu zenu kubwa, na unaweza kutumiwa kama injini ya kusukuma mbele uchumi wenu. Maelfu ya watalii wanaokuja hapa kutoka sehemu zote duniani hawaji tu kwa sababu ya fukwe zenu zinazovutia. Wanakuja pia kwa sababu wanajua kuna kitu cha kipekee kwenye visiwa hivi; watu wenyewe ni watu wa kipekee, na kwamba kuna historia muhimu hapa visiwani. Na kama mtahifadhi historia hiyo, mtakuwa mmeitunza kwa ajili yenu, watoto wenu, wajukuu wenu, na kwa ajili ya watalii pia.

  • Kwa hiyo ninawashukuru sana kwa kuweza kuja hapa kutusaidia kuwaelimisha wengine kuhusu historia na utamaduni wa Zanzibar; na ninawapeni pongezi kwa kufanikisha mradi huu muhimu.

  • Mheshimiwa waziri, Mabibi na Mabwana, asanteni na tutaonana tena!