Skip Navigation
You Are In: Home > Habari Kutoka Ubalozi > Kiswahili Speeches > Hotuba ya Kaimu Balozi wa Marekani Larry André kwenye Uzinduzi wa Programu ya Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU ya ANGAZA ZAIDI
Skip Left Section Navigation

Speeches

Uzinduzi wa Programu ya Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU ya ANGAZA ZAIDI

Mahali: Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam

Aprili 28, 2009

Hotuba ya Kaimu Balozi wa Marekani Larry André

Watu wa Marekani na watu wa Tanzania ni wabia madhubuti katika vita dhidi ya VVU/UKIMWI, na AMREF ina jukumu muhimu sana katika ubia huo. Fedha kwa ajili ya utekelezaji wa programu ya Angaza Zaidi zimetolewa na watu wa Marekani kupitia PEPFAR, ambao ni Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Mapambano dhidi ya UKIMWI. PEPFAR ni mfuko mkubwa zaidi wa kiafya wa kimataifa uliowahi kutengwa na taifa moja kwa ajili ya mapambano dhidi ugonjwa mmoja.

Mafanikio ya mpango huu yanapimwa kwa mamilioni ya Watanzania ambao wamepatiwa huduma za upimaji wa hiari na ushauri nasaha, mamilioni ambao wamepatiwa huduma za matibabu na mamilioni ambao wameelewa na kuufanyia kazi ujumbe wa kujikinga dhidi ya maradhi haya.

Huduma za Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU/UKIMWI huwawezesha Watanzania kushiriki katika mapambano dhidi ya janga hili kubwa kwa kujua hali za afya zao na kasha kuchukua hatua mwafaka za kudhibiti kuenea kwake. Tuna fahari kubwa kuwa na ubia na watu na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa huduma hizi muhimu zinapatikana kwa Watanzania wote.

AMREF Tanzania inapokea tuzo mpya ya miaka mitano kutoka kwa watu wa Marekani ili kuboresha na kupanua zaidi huduma zake za Ushauri Nasaha na Upimaji kwa kuzingatia uzoefu na mafunzo yaliyopatikana katika Mradi wa Angaza na Kampeni ya Kitaifa ya Ushauri Nasaha na Upimaji wa Hiari ya mwaka 2007 iliyoongozwa na Rais Kikwete. Mtukufu Rais: wewe na Mama Kikwete mmeonyesha njia. Toka mlipojitokeza hadharani na kupima VVU, zaidi ya Watanzania milioni 4 wamefuata nyayo zenu na kupima kwa hiari. Tunapongeza uongozi na ushawishi wako katika nyanja zote za mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI na unyanyapaa unaoambatana na tatizo hili.

Kwa kuzingatia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka nane iliyopita, tunaamini kuwa vijana na watu wazima watakaokwenda katika vituo vya Angaza Zaidi watapata huduma zenye kiwango cha juu cha ubora na watahudumiwa kwa upole, huruma na uchangamfu na timu ya washauri nasaha wenye uzoefu mkubwa ya Angaza Zaidi.

Wabia katika utekelezaji wa Mradi wa Angaza Zaidi ni wengi, wakiwakilisha wanaharakati wa aina mbalimbali katika mapambano haya. Wabia hawa, wanaofanya kazi katika pembe zote za nchi kuanzia Mkoa wa Kagera hadi mikoa ya kusini ya Rukwa na Ruvuma, ni pamoja na serikali za mitaa, hospitali, mashirika ya kidini, mashirika yasiyo ya kiserikali na wawakilishi wa sekta binafsi. Kwa kufanya kazi pamoja tunakuwa na nguvu zaidi katika mapambano haya. Angaza Zaidi ni mojawapo ya mifano bora ya ubia unaohitajika ili kuwawezesha watu mmoja mmoja, familia na jamii kukabiliana na kuzishinda changamoto za VVU/UKIMWI.

Tunaamini kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kama AMREF Tanzania yana jukumu muhimu katika kujenga jamii imara na yenye afya bora. Ubia wetu madhubuti na Serikali ya Tanzania, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na mashirika yasiyo y kiserikali ya Kiafrika kama AMREF ni sehemu ya maono yetu ya kuwa na Afrika isiyo na VVU na UKIMWI. Tunawapongeza wale wote wanaofanya kazi bila kuchoka katika kuifanya ndoto hii kuwa hali halisi.

Sera na programu imara za afya mahali pa kazi ni nguzo muhimu ya mfumo wa afya wa Marekani. Tunaipongeza AMREF kwa kuendelea kuweka msisitizo katika uanzishaji wa ubia mpya kati ya sekta binafsi na sekta ya umma kama ilivyojidhihirisha katika ubia kati ya Angaza Zaidi na makampuni kama Geita Gold Mines na Barrick Tanzania. Kwa kufanya kazi kwa ubia na Wizara ya Afya na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI, AMREF na wabia wake katika sekta binafsi wameonyesha mfano mzuri katika kutekeleza kwa vitendo wajibu wa kijamii wa mashirika na makampuni binafsi, jambo linalohimizwa sana katika ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi nchini Tanzania.

Tunatoa wito kwenu nyote, kuitumia fursa hii, kujua bila malipo yoyote, hali zenu za maambukizi ya VVU na kuwahamasisha marafiki na watu wa familia zetu kujitokeza ili nao waweze kupima afya zao. Ni baada tu ya kupima na kujua hali yako ndipo unapoweza kupanga vyema maisha yako ya baadaye. Iwapo utagundulika kuwa na VVU, basi jiandikishe katika mojawapo ya vituo 80 vya matibabu vilivyofunguliwa nchini kote Tanzania. Hali kadhalika, kama tayari unaishi na VVU, jifunze namna unavyoweza kuishi kwa matumaini ukiwa na afya njema na kuwasaidia wengine kuishi kwa matumaini.

Unaweza kabisa kuamua, mustakabali na hatima ya maisha yako ya siku zijazo. Elewa hali yako ya afya na uwe kiongozi katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Iwapo tunaishi na VVU au la ni wajibu wa kila mmoja wetu kuamua kwa dhati kuishi maisha yatakayotuwezesha kuwa na afya bora.

Kwa niaba ya watu wa Marekani, ninapenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe Mheshimiwa Rais, kuwashukuru watendaji wote wa serikali yako na rafiki zetu wa AMREF kwa jitihada kubwa mnazozifanya, kwa niaba ya ubia kati ya Tanzania na Marekani, katika kuboresha afya ya wananchi wa nchi hii. Tutaendelea, bila kuchoka, kufanya kazi pamoja na taifa lote la Tanzania ili kufikia maono ya Rais Kikwete ya kuwa na “Tanzania bila UKIMWI." Tunaamini inawezekana.

 

TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA.
AHSANTENI SANA.

 
Article translated in: