Speeches
Hotuba Ya Balozi Wa Marekani Michael Retzer Kwenye Warsha Ya Agoa.
Kuimarisha uwezo na ushindani wa Tanzania katika biashara.
Venue:Kempinski Kilimanjaro Hotel, Dar es Salaam
Mei 11, 2006
Karibuni. Habari zenu? Mheshimiwa Waziri Karamagi, wawakilishi wa Serikali ya Tanzania, na wadau kutoka sekta binafsi ya Tanzania, habari za asubuhi kwenu wote na karibuni sana. Ninafurahi kuwa hapa leo, kufungua mkutano huu wa kusisimua; mkutano ambao lengo lake ni kuweka msukumo na ubunifu katika juhudi za kuboresha uwezo wa kibiashara wa Tanzania.
Ningependa kuwakaribisha kimaalum wafanyabiashara wote ambao wameungana nasi hapa leo. Kama mtu anayetoka kwenye sekta binafsi, ningependa kusisitiza kwamba serikali hazitengenezi utajiri, wajasiria ndiyo wanaofanya hivyo.
Serikali zinaweza kuisaidia sekta binafsi, kwa kuhakikisha kwamba kuna mazingira mazuri ya usimamizi, miundombinu ya kutosha na uwazi, lakini ni nyinyi wote hapa – wajasiriamali – ambao ndiyo injini inayosukuma mafanikio ya biashara na uchumi.
Katika uchumi wa dunia ya leo wenye ushindani mkali, ni kitu gani kinahitajika kwa kampuni binafsi au sekta binafsi ya nchi kuwa na ushindani? Kimsingi, mjasiriamali lazima awe na uwezo wa kupeleka bidhaa bora kwenye masoko ya nje kwa bei nafuu.
Tunatambua kwamba kuna changamoto kubwa zinazokabili nchi zinazoendelea, kama vile Tanzania, hususan katika kuimarisha uwezo wa biashara na kuwa na ushindani katika masoko ya dunia.v Katika mtazamo wa marekani, ambao ninaamini unachangiwa na washiriki wetu kutoka Tanzania, uboreshaji wa uwezo wa Tanzania katika biashara si kwamba tu unafaa kuimarisha uchumi, bali ni kitu cha lazima.
Moja ya malengo ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania yanayopewa kipaumbele ni kuchochea maendeleo. Kufanikisha lengo hili, Serikali ya Marekani kwa sasa inatoa takriban dola milioni 200 kila mwaka kusaidia vita dhidi ya UKIMWI na ugonjwa wa malaria; kuboresha utawala bora, kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kuhakikisha kwamba kuna utunzaji endelevu wa mazingira.
Pamoja na kwamba tunafanya juhudi madhubuti kutoa misaada ya maendeleo, tunaamini kwa dhati kuwa biashara ndiyo nguzo imara ya kuhakikisha uchumi wa Tanzania unazidi kukua. Waziri wa Mambo ya Nje Condoleezza Rice alifafanua vizuri dhana hii aliposema:
“Misaada ya maendeleo inaweza kuwa chachu. Lakini peke yake haiwezi kuwawezesha wananchi kujitoa kwenye umaskini. Masoko huru yanayoruhusu watu binafsi kuvuna faida za kufanya kazi kwa bidii ni kitu cha lazima.”
Mpango wa AGOA (The African Growth and Opportunity Act) umetokana na dhana hii. Kama wengi wenu mnavyofahamu, mpango wa AGOA SIYO mkataba wa biashara huru na wala SIYO makubaliano yanayohusisha nchi kadhaa.
Mpango wa AGOA ni sheria ya Marekani iliyopitishwa na Bunge la Congress mwaka 2000 inayoruhusu nchi za Kiafrika zinazostahili, kuuza bidhaa zao bila ushuru au mpaka wa kiasi, katika soko la Marekani.
Hivi sasa mpango wa AGOA unahusisha aina ya bidhaa zaidi ya 4,500, kuanzia magari, mananasi, mpaka fulana za T-shirt na maua aina ya rose. Hivi sasa zaidi ya asilimia 98 ya bidhaa zinazoingia katika soko la Marekani kutoka Afrika hazitozwi ushuru.
Mpango wa AGOA umefungua mlango wa kujenga uhusiano mpya wa kibiashara na hivyo kuwezesha biashara kati ya Marekani na nchi za Kiafrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 50. Mwaka jana, thamani ya bidhaa za AGOA (bila kuhesabu mafuta) zilifikia zaidi ya dola bilioni 2.5.
Hata hivyo umuhimu wa wa AGOA ni zaidi ya takwimu na ongezeko la asilimia ya bidhaa zinazoingia Marekani kutoka Afrika. Sheria ya AGOA inadhihirisha kuibuka kwa mtazamo mpya unaoondokana na dhana ya utegemezi na badala yake kukumbatia maendeleo ya kiuchumi katika misingi ya soko huria. Mpango wa AGOA unaashiria kutambua kwa Marekani kwamba, nchi kama Tanzania ni wabia halisi wa kiuchumi na kwamba ni nchi ambazo zinafaa kufanya nazo biashara.
Tanzania ilijiunga na mpango wa AGOA mwaka wa 2002. Katika mwaka wa 2005, jumla ya mauzo ya Tanzania nchini Marekani yalipanda kutoka dola milioni 24.2 hadi dola milioni 33.7. Ongezeko hili liliifanya Tanzania kuwa moja ya nchi saba zilizoweza kupanua mauzo yake chini ya mpango wa AGOA katika mwaka wa 2005.
Katika kiwango cha uchumi mdogo mdogo, kumekuwepo na mafanikio muhimu nchini Tanzania, na hivyo kudhihirisha uwezekano wa nchi hii kuingia katika soko la Marekani – soko ambalo siyo tu kwamba ni kubwa zaidi kuliko yote duniani [dola trilioni 11], bali pia ni soko gumu sana kueleweka.
Kwa mfano, katika mwaka wa 2005, bidhaa zilizotengenezwa kwa mkono na wanawake wajasiriamali wachache wenye bidii zilipata wateja wakubwa kama vile Smithsonian na Target. Hivi karibuni nilisikia kwamba kampuni moja inayotengeneza samani jijini Dar-es-Salaam imefanikiwa kuuza nchini Marekani samani zinazotumiwa barazani.
Pamoja na mafanikio haya, kiwango cha mafanikio ya mpango wa AGOA nchini Tanzania siyo kikubwa kwa maana ya kiasi cha mauzo na kwa kulinganisha na nchi jirani kama vile Kenya, Uganda, Malawi na Ethiopia. Kusema kweli, bado sijaridhika kwamba mpango wa AGOA umetumiwa kikamilifu au umezaa matunda kwa kiwango kinachotakiwa nchini Tanzania.
Serikali ya Marekani inatambua kwamba mpango wa AGOA ni kama tofali la kujengea na siyo silaha. Kuendeleza juhudi za mpango wa AGOA, Rais Bush alitangaza hivi karibuni mpango mpya wa kuboresha ushindani - The African Growth and Competitiveness Initiative – mpango wa miaka mitano uliotengewa dola milioni 200 kujenga uwezo na ushindani wa nchi za Afrika katika biashara.
Ingawa kuna fursa nyingi kwa Tanzania kupanua uwezo wake wa kufanya biashara na Marekani, Tanzania pia ina nafasi pia ya kuimarisha uhusiano wake wa kibiashara na nchi kama zile za Umoja wa Ulaya, India, China, pamoja na nchi jirani katika Afrika ya Mashariki na Kusini. Ufunguo ni kuiwezesha Tanzania kukuza uwezo wake wa kibiashara na kunoa makali yake ya ushindani katika masoko ya nchi jirani na yale ya kimataifa.
Ninaamini wote hapa tunafahamu mgongano uliopo katika taswira ya biashara ya Tanzania: Fursa kubwa; vipingamizi vikubwa. Hii ni taswira halisi ya mgongano.
Kwa upande mmoja, Tanzania imejaa fursa nyingi za kuuza bidhaa nje: rasilimali kubwa ya madini, wanyama pori wengi na wa aina mbalimbali, vito vya thamani, hazina kubwa ya mazao ya kilimo ambacho hakijaendelezwa kikamilifu, n.k.
Kwa upande mwingine, kuna orodha ndefu ya vipingamizi: uwezo hafifu wa kuzalisha, miundombinu duni, ukosekanaji wa mikopo, uwezo wa kukidhi viwango vya kimataifa vya ubora n.k.
Hizi ndizo pande mbili za hali halisi kuhusu uwezo wa kibiashara wa Tanzania katika soko la dunia: vipingamizi vingi na maeneo mengi yenye fursa. Kwa hiyo swali siyo kama Tanzania inaweza kuwa na uwezo wa kushindana, bali ni jinsi gani Tanzania inaweza kuwa na uwezo wa kushindana.
Na ndiyo maana tumeandaa mkutano huu:
Kujifunza jinsi wajasiriamali wanavyoweza kuvishinda vipingamizi mbalimbali vinavyozuia mauzo ya nje;
Kuangalia jinsi wajasiriamali wanavyoweza kusafirisha bidhaa zenye ushindani kwenye masoko makubwa na magumu kama lile la Marekani.
Na kuchunguza jinsi gain sisi sote tunaweza kuchangia kwa ufanisi zaidi kuimarisha biashara nchini Tanzania.
Hebu ngoja niwaache na wazo la mwisho kuhusu nguvu ya bishara na ahadi inayobeba katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara:
Kwa mujibu wa Tume ya Blair, sehemu ya bara la Afrika katika bishara ulimwenguni ni takribani asilimia 2, ikiwa imeshuka kutoka asilimia 8 wakati wa miaka ya 1960. Ikiwa sehemu ya Afrika katika biashara ya dunia itaongezeka kutoka asilimia 2 hadi 3 tu, ongezeko la kipato cha nchi za Kiafrika litazidi dola bilioni 70. Hii ni mara tatu ya thamani ya jumla ya misaada yote ya maendeleo kutoka kwa wafadhili. Mara tatu.
Asanteni kwa kushiriki katika hafla hii. Ninawashukuru kwa kutumia muda wenu kuchangia uzoefu na ujuzi wenu kuhusu mada hii muhimu. Ninaamini kwamba kubadilishana huku kwa mawazo kutasaidia kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini Tanzania.
Asanteni sana.



