Speeches
Mkutano wa kanda kuhusu haki miliki ubunifu (Intellectual Property Rights)
Venue: Movenpick Hotel, Dar es Salaam
Oktoba 11, 2007
Hotuba ya Balozi wa Marekani - Mark Green
Nilifurahi kupata mwaliko wa kutoa hotuba ya kufunga mkutano huu. Ningependa kuwapongeza kwa kuufanya mkutano huu uwe wa mafanikio, kupitia majadiliano ya wazi ambayo ni hatua muhimu katika kufikia malengo yetu ya pamoja ya kulinda miliki ubunifu (intellectual property) na kupambana na bidhaa feki. Maoni yangu ni kwamba, katika kipindi cha siku chache zilizopita, mmweza kushiriki mkutano huu kwa dhati.
Ningependa kuishukuru sana Tume ya Ushindani (Fair Competition Commission) ya Serikali ya Tanzania, na Chama cha Wafanyabiashara wa Marekani na Kenya (American Chamber of Commerce of Kenya), kwa kutumia muda wenu na juhudi zenu kuandaa mkutano huu. Pia ninawapongeza wawakilishi wa sekta binafsi kwa kuja hapa kujadili mada hii muhimu.
Tumekutana pamoja hapa Dar-es-Salaam kwa sababu wote tunaamini kwamba, haki miliki ubunifu (intellectual property rights) ni jukumu la kila mtu – na jukumu hilo haliishii mpakani. Kulinda haki miliki ubunifu kuna manufaa kwa jamii katika kila ngazi, na ni suala la kikanda na kimataifa. Ninafurahi kwamba waandishi wa habari wameungana nasi, kwa sababu ningependa waweze kuelezea umma, tuna maana gani tunaposema “haki miliki ubunifu. “Haki miliki ubunifu inatumika kwa kazi au bidhaa ambazo hazishikiki (intangible goods), lakini hata hivyo zina thamani. Mifano mizuri ni pamoja na: programu za kompyuta, teknolojia, muziki, filamu, vitabu, usanifu majengo, aina za mapishi, na siri za biashara.
Lengo la kulinda miliki ubunifu ni kuzipa heshima na umakini ule ule bidhaa hizo, kama vile tunavyozipa mali zetu. Mtu wa kwanza kubuni (creator) anaweza kutoa haki ya kununua, kuuza, kutoa leseni, na kuhamisha miliki ubunifu. Ubunifu una haki ya kulindwa kama vile zinavyolindwa nyumba zetu, magari yetu, au mali zetu zingine.
Katika dunia ambayo mawazo (ideas) ndiyo sarafu yetu wote, wizi wa miliki ubunifu unaweza kuathri kwa urahisi uchumi wa nchi, pamoja na sura halisi ya utamaduni wake. Sheria za hataza (patent laws) zinahamasisha uvumbuzi wa bidhaa mpya na zilizoboreshwa, pamoja na michakato. Wakati huo huo, zinahakikisha kwamba kuna uhuru mkubwa wa umma kupata taarifa kuhusu bidhaa na michakato hiyo mipya.
Sheria za hataza zinahamasisha ubunifu wa kazi za uandishi, programu za komputa, kazi za sanaa, na udhihirisho wa utamaduni wa taifa. Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO), liliandaa warsha kwa wasanii na wanamuziki wa Tanzania, ambayo iliwafungua macho wengi wao. Badala ya kufurahia tu umaarufu wanaoupata wakisikia nyimbo zao zikipigwa kwenye vituo vya redio, wanamuziki walijifunza kwamba, kazi zao zinaweza kuwaletea faida kubwa kama zitawekewa sawasawa hakilimiliki na kulindwa.
Sheria za nembo za biashara (trademark laws) zinahamasisha kuendeleza na kudumisha bidhaa, pamoja na huduma za ubora wa hali ya juu, na pia kuzisaidia kampuni kujenga uhusiano mzuri na wateja wao. Kama nembo za biashara zisingekuwa zinalindwa, mteja asingekuwa na uhakika kama viatu vya mpira alivyovaa ni kweli vimetengenezwa na kutangazwa na mwanamichezo nyota anayempenda; au kama kweli maji ya chupa anayokunywa mteja ni masafi; au kama kweli dawa anazompa mzazi mtoto wake zimetengenezwa kihalali na kampuni iliyoandikwa kwenye bidhaa hiyo.
Soko linaweka thamani kubwa kwenye aina zote hizi za miliki ubunifu - - thamani ambayo inapaswa kulindwa. Kushindwa kulinda miliki ubunifu kunazuia ubunifu na kudumaza kukua kwa uchumi, pamoja na uwekezaji. Katika mfano ule wa dawa au chakula, kukosekana kwa ulinzi wa miliki ubunifu kunaweza kuleta athari au mambo mabaya zaidi.
Udhaifu katika ulinzi wa haki miliki ubunifu unawafanya wasanii, wavumbuzi, na wabunifu wasiweze kuwa na haki juu ya matumizi ya vitu walivyotengeneza. Kulinda haki miliki ubunifu kunawahamasisha watu, wawe wachoraji wa picha za tinga tinga, au wasanii nyota wa bongo fleva, katika nchi yoyote ile, kuendelea kubuni na kuendeleza mawazo mapya na mwelekeo mpya.
Ulimwenguni kote, wasanii wanaanza kuelewa umuhimu wa kulinda kazi zao. Watengeneza filamu wa Hong Kong, ambao hapo awali walikuwa wakipata hasara za kiuchumi kutokana na wizi wa filamu zao, walifanikiwa kuhamasisha serikali kuchukua hatua kulinda kazi zao. Tangu mwaka 2004, vikundi kadhaa vya wasanii vimejaribu kushinikiza ili pawe na ulinzi zaidi wa miliki ubunifu. Wasanii hao ni pamoja na wanamuziki kutoka Ethiopia, na watengeza filamu wa Bangladesh.
Mamilioni ya dola hupotea kupitia uuzaji wa nakala haramu za picha za DVD. Hatuna budi kuwafundisha vijana wetu kwamba, ni makosa kununua bidhaa feki.
Wale wanaokiuka haki miliki ubunifu hawana motisha wa kukidhi viwango, au kuhakikisha kuwa bidhaa zao zina ubora unaotakiwa. Bidhaa feki zinaweza kuua. Huko nchini Niger, mwaka wa 1995, zaidi ya watu 2,500 walikufa baada ya kupewa chanjo feki za kuzuia ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo (meningitis). Huko Marekani, mwanzoni mwa mwaka wa 2004, mwanamume mmoja alikiri kosa la kuuza dawa feki za kuua wadudu waharibifu, dawa ambazo zilikuwa zinatumika kudhibiti mbu waliokuwa wakieneza virusi vinavyosababisha homa ya West Nile. Na mwezi Mei 2004, mamlaka za serikali ya Uchina zilisema kwamba idadi kubwa ya watoto walikufa kutokana na kupewa chakula feki cha watoto wachanga.
Daima utafiti huonyesha kuwa, kuna uhusiano kati ya kulinda miliki ubunifu na kukua kwa uchumi wa nchi. Takriban asilimia 70 ya uzalishaji wa kiuchumi duniani unatokana na huduma, ambazo nyingi hutegemea kwa kiasi kikubwa teknolojia na uvumbuzi mbalimbali, ambao unaweza kuitwa miliki ubunifu. Ripoti ya maendeleo ya uchumi wa dunia ya 2002 (Global Economic Prospects Report 2002) ilionyesha kuwa, “katika viwango vyote vya mapato, haki miliki ubunifu zinahusishwa na kuongezeka kwa uwekezaji wa biashara na wa nje, na hii inachochea kukua haraka kwa uchumi.” Uhusiano huu ni kitu ambacho Tanzania na nchi jirani katika ukanda huu zinaweza kuutumia ili kufanikisha juhudi za kuwavutia wawekezaji kutoka nje.
Kila mtu ana maslahi katika kulinda miliki ubunifu – mvumbuzi ana haki ya kufaidika na mavuno ya kifedha ya uvumbuzi wake; mlaji au mteja anastahili kujua kama bidhaa anayonunua, au watoto wake wanaoitumia, ni halisi (siyo feki); na makampuni yanahitaji utengemano katika shughuli zao, ili kuhalalisha uwekezaji wao. Serikali pia zinapoteza kiasi kikubwa cha mapato kwa kukosa kukusanya kodi mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara halali wanaopoteza soko lao kwa watu wanaouza bidhaa feki.
Njia ya kusonga mbele katika juhudi za kulinda haki miliki ubunifu ni pamoja na kuelimisha umma, jinsi bidhaa feki zinavyomuathiri kila mtu. Tunapaswa kuimarisha sheria na adhabu, ili makampuni yaweze kuandaa mipango yao na marekebisho kuhusu teknolojia na ubunifu mpya. Tahariri, kama ile iliyoandikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ushindani, Bwana Godfrey Mkocha, mwezi uliopita, ni njia bora ya kukabiliana na fikra potofu. Bwana Mkocha alieleza wazi tofauti muhimu kati ya bidhaa halali zinazoheshimu haki miliki ubunifu, na bidhaa feki zenye bei rahisi – pamoja na hatari zinazohusiana na bidhaa feki. Tunapaswa kuendelea kuhamasisha vyombo vya Habari, na kutafuta njia mpya za kueneza ujumbe ulio wazi na sahihi kwa umma.
Katika moyo huo huo, tumesisimka kuona jinsi Bunge litakavyopitia upya sheria iliyopo ya kudhibiti bidhaa feki, kwenye kikao chake kijacho cha mwezi Novemba. Tunavyofanya kazi pamoja, kupitia mifumo mbalimbali, ni vizuri kama tukichukua hatua kuendeleza njia mpya za kulinda haki miliki ubunifu, pamoja na kupiga vita bidhaa feki. Kulinda miliki ubunifu ni fursa nyingine ya kushirikiana katika kuhifadhi kazi zetu za kisanii na kitamaduni, na kuhakisha kuwa uchumi unakua kwa njia endelevu.
Kwa kumaliza, ninatambua kuwa mikutano kama hii ni chachu muhimu ya majadiliano, siyo tu kuhusu masuala yanayotukabili wote kuhusu haki miliki ubunifu na bidhaa feki, lakini muhimu zaidi, inatupa fursa ya kujadili jinsi tunavyoweza kufanya kazi pamoja kumudu changamoto hizo.
Huu ni wakati wa kihistoria katika uhusiano kati ya Marekani na Tanzania. Kuidhinishwa kwa msaada wa mfuko wa Millennium Challenge ni hatua ya Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia katika awamu mpya ya uhusiano wetu. Wote tumeahidi kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu, ili kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kuiwezesha Tanzania kuvutia wawekezaji wengi zaidi. Kutoa ulinzi thabiti kwa haki miliki ubunifu ni hatua muhimu katika kufanikisha lengu letu hilo la pamoja.
Napenda tena kuwashukuru kwa kuhudhuria mkutano huu. Ninaamini kwa dhati kwamba, ni jambo muhimu kukutana uso kwa uso kujadili na kuratibu mikakati yetu, ili tuweze kupata ufumbuzi wa pamoja kuhusu suala hili. Niliwasili hapa nchini takriban mwezi mmoja uliopita. Lakini ninatoa ahadi kwa jamii ya wafanyabiashara hapa, na kwa Serikali ya Tanzania kwamba, wakati wote nitakapokuwa nchini hapa kama mwakilishi wa wananchi wa Marekani, nitafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na ninyi, huku tukikabiliana na kumudu suala la bidhaa feki, na kuhakikisha kuwa tunalinda sawasawa miliki ubunifu.



