Speeches
Sherehe ya mahafali ya wanajeshi wa kulinda amani wa Jeshi la Wananchi Tanzania
Mahali: Airwing
Ijumaa, Desemba 7, 2007
Hotuba ya Balozi Mark Green (kama ilivyotayarishwa)
Ni heshima kubwa kwangu kuwa hapa kwenye mahafali ya kwanza ya wanajeshi waliopata mafunzo yao hapa nchini Tanzania, chini ya mpango wa kutoa misaada ya mafunzo barani Africa ACOTA (African Contingency Operations Training Assistance). Ningependa kuwapongeza siyo ninyi tu; lakini pia wanajeshi wenzenu ambao ninyi mnakwenda kuchukua nafasi zao hivi karibuni kule Lebanon - nao pia wanastahili pongezi. Wao, pamoja na wanajeshi wengine kutoka Afrika wanaolinda amani, wamekuwa wakifanya kazi muhimu sana katika kuleta utengamano barani Afrika, na ulimwenguni kote.
Ninyi wote mnafuata desturi yenye heshima ya kulinda amani. Kwa muda mrefu, Waafrika wamedhihirisha moyo wa kweli wa kujitoa na azma ya kweli, kuhusiana na masuala ya upatanishi pamoja na utatuzi wa migogoro. Ni wazi kuwa, Waafrika wamekuwa wakibeba sehemu yao ya mzigo katika kufanikisha mikakati ya kimataifa ya kulinda amani na usalama. Hivi sasa, Waafrika wanatoa zaidi ya theluthi moja ya walinda amani wote ulimwenguni, na mahitaji ya kuwa na walinda amani waliopata mafunzo halisi na wenye vifaa vinavyotakiwa ni kubwa kulipo hapo awali.
Tangu 1977, mafunzo na misaada inayotolewa na Marekani imekuwa ikitekelezwa kupitia mpango wa ACOTA. Uamuzi wa kujiunga na mpango huu na kutumia majeshi yaliyopitia mafunzo ya ACOTA, ni uamuzi huru wa kitaifa wa kila nchi inayoshiriki, lakini ni mchakato ambao Marekani inauhamasisha.
Ningependa kuupongeza uongozi wa Rais Kikwete, Waziri wake wa Ulinzi pamoja na Mkuu wa Majeshi, kwa kukubali mafunzo haya. Kwa kutumia makubaliano ya mpango wa ACOTA kati ya Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marekani iliweza kuendesha mafunzo haya kufuatia ombi la JWTZ, katika kipindi cha chini ya wiki sita. Tuna shauku kutoa fursa zaidi za mafunzo hapo mbeleni.
Ili Afrika iweze kudumisha amani, nyumbani na nje ya mipaka yake, hatuna budi kuhakikisha tunaweka mifumo imara ya kiusalama. Mpango wa ACOTA unatoa kwa jeshi husika mikakati mingi ya kusaidia kulinda amani. Na lengo la ACOTA ni kusaidia na kuimarisha juhudi za Umoja wa Ulaya, NATO, na juhudi za washiriki wetu za kutoa mafunzo ya kulinda amani.
Marekani ina imani kubwa katika mpango wa ACOTA. Katika mwaka wa 2007, tuliweka zaidi ya dola milioni 70 kwenye mpango huu, hii ikiwa ni takriban mara mbili ya kiasi tulichowekeza mwaka 2006.
Tangu uanzishwe, mpango wa ACOTA umetoa mafunzo kwa walinda amani zaidi ya 92,000 kutoka majeshi ya nchi za Afrika tunazoshirikiana nazo, na lengo letu ni kutoa mafunzo kwa walinda amani 228,000 ifikapo 2010. Mpango wa ACOTA umetoa mafunzo kwa vitendo kwa walinzi wa amani kutoka Afrika, pamoja na mafunzo ya ukamanda na unadhimu na mazoezi kwa vikosi, brigedi, na wafanyakazi wa makao makuu ya majeshi ya kimataifa. Tunaona fahari kufanya kazi sasa pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kama washiriki, kuhakikisha ufanisi wa jeshi la Umoja wa Mataifa linalolinda amani Lebanon, (United Nations Interim Force in Lebanon) UNIFIL, pamoja na majukumu mengine ya kulinda amani hapo mbeleni.
Taifa langu lilifurahi wakati Jeshi la Wananchi wa Tanzania lilipopeleka kikundi cha Polisi Wanajeshi (Military Police) 77 mapema mwaka huu huko Lebanon kama sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani huko Lebanon UNIFIL. Kikosi hiki kimekuwa huko tangu February, na ninyi mtaendeleza kwa heshima jukumu hilo muhimu.
Taifa langu limetiwa moyo pia na kauli za Tanzania kuwa itaendelea kupeleka kikundi kimoja cha Polisi Wanajeshi (Military Police) kwenye shughuli za Umoja wa Mataifa za kulinda amani nchini Lebanon, kwa muda wote ambao jeshi hilo litaendelea kuhitajika huko.
Tunawashukuru Watanzania kwa kuendelea kuunga mkono harakati hizi, ili kuleta utengemano katika nchi ya Lebanon iliyoharibiwa vibaya na vita, na kuleta usalama wa kiwango cha juu kwa wananchi wake na serikali yao. Kuwepo kwa walinda amani wa JWTZ wanaoleta utengemano nchini Lebanon kutakuwa na manufaa ya kudumu katika sehemu hiyo ya dunia.
Marekani itaendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha uwezo wa Waafrika kuendesha shughuli za kusaidia kulinda amani. Kwa niaba ya taifa langu, ningependa tena kuwapongeza ninyi na kuwatakia mafanikio katika kutekeleza kazi yenu na mrudi salama nyumbani.
Asanteni sana!



