Kiswahili Speeches
Uzinduzi wa Petterson House
MAHALI: 8 Mazizini, Unguja
Alhamisi, Desemba 13, 2007
Hotuba ya Balozi Mark Green
Asalam Alaykum!
Hebu niwe mtu wa kwanza kuwakaribisheni rasmi kwenye Petterson House.
Tuko hapa asubuhi ya leo kumuenzi Balozi Petterson, lakini pia kuenzi na kutambua uhusiano wa kihistoria kati ya Marekani na Zanzibar.
Ninapenda kumshukuru Balozi Mdogo Purnell kwa kutupa historia fupi ya uhusiano kati ya Marekani na Zanzibar. Hafla hii asubuhi ya leo imefanikishwa kwa kiasi kikubwa kupitia juhudi zake.
Licha ya kutokuwa hapa Zanzibar rasmi tangu 1979, nafikiri mtakubali kuwa Marekani imeendelea kuwa hapa tangu wakati huo… uwepo wa manufaa ambao unaleta tofauti.
Maofisa kutoka Ubalozi wa Marekani huwa wanasafiri kuja hapa karibu kila siku, na ninaamini wengi wenu mnamfahamu Mussa Shehe, msaidizi wetu wa masuala ya kisiasa na ya umma, ambaye anafanya kazi nasi hapa Zanzibar.
Tukienda mbele, tuna mpango wa kuweka Mmarekani hapa, kwa karibu muda wake wote, kuanzia mapema mwaka kesho kwa sababu ya shughuli nyingi tunazofanya Zanzibar.
Kuna miradi mingi sana inayotekelezwa na Marekani, siwezi kuielezea yote kwa kina. Kwa mfano, kupitia mfuko wa Balozi wa kuhifadhi utamaduni, Marekani imesaidia kukarabati misikiti miwili Pemba; imekarabati nyumba ya makumbusho ya Chake Chake, iliyo kwenye ngome ya karne ya 18; na kusaidia kuhifadhi muziki wa Taarab.
Mfuko wa Balozi wa kusomesha wasichana unasaidia kugharamia elimu ya wasichana takriban 300 wa Zanzibar, kuanzia elimu ya msingi hadi kumaliza masomo ya sekondari.
Pia tumechangia katika kutoa kompyuta mashuleni, pamoja na kutoa mafunzo ya lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi zaidi ya 100. Ni matumaini yetu kuwa, mafunzo hayo yatawapa wanafunzi fursa bora zaidi ya kuendelea na masomo yao, au kupata ajira. Pia tuna mtaalamu wa lugha ya Kiingereza ambaye anaimarisha ujuzi wa waalimu Wazanzibari wanaofundisha lugha hiyo.
Juhudi zetu za kuboresha elimu pia zimeimarishwa kupitia kipindi cha elimu kwa redio cha RISE, na miradi ya CREATE, pamoja na ule wa kutunza mazingira kwenye maeneo ya pwani. Pamoja na kituo chetu chaAmerican Corner kilichopo kwenye Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), hivi karibuni tunategemea kuweka saini mkataba na Wizara ya Elimu wa kuanzisha kituo cha pili cha American Corner huko Pemba.
Pia tunashirikiana na wenzetu katika sekta ya afya kupitia mpango wa Rais wa kupambana na malaria (PMI – Presidential Malaria Initiative). Mpango huu wa PMI umepata mafanikio makubwa hapa Zanzibar. Kipindi kama hiki mwaka jana, Katibu Mku wa Wizara ya Afya, Dk. Jiddawi, aliungana na Rais Bush kwenye mkutano Ikulu ya Marekani, ambao ulisifia mafanikio ya kihistoria ya mpango huo.
Kama mnavyoona, Zanzibar ni muhimu kwa wananchi wa Marekani. Tuna shauku kubwa kuona mchakato wa usuluhishi visiwani Zanzibar ukimalizika haraka na kwa amani.
Watu wanaweza kusema kuwa 2010 bado iko mbali, lakini tuko karibu kuingia 2008, na kufumba na kufumbua, uchaguzi ujao utakuwa umewadia. Ni lazima tujikumbushe kuwa mazungumzo ya muafaka kati ya Chama cha Mapinduzi na Chama cha Wananchi cha CUF yalianza Zanzibar takriban mwaka mmoja uliopita, yaani tarehe 17 Januari 2007.
Mazungumzo haya yamendelea kwa kipindi cha mwaka mzima. Yalipokwama mwezi wa Agosti mwaka huu, pande zote mbili zilikubaliana kuweka juhudi mpya.
Pamoja na kuwa tumefurahi kuona kwamba mazungumzo yamekwenda mbele, wakati huohuo ningependa kuzitia moyo pande zote mbili kufanya juhudi za dhati kufikia makubaliano ya haki - - makubaliano ambayo yataruhusu muda wa kutosha kuyatekeleza.
Ninapongeza juhudi za dhati za Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa majadiliano haya yanaendelea. Ni matumaini yetu kwamba, makubaliano ya haki yatapatikana, ambayo yatahakikisha kuwa taasisi za kidemokrasia zinaendelea kukua hapa Zanzibar.
Bila shaka, muafaka siyo suala pekee linaloongelewa na Marekani hapa. Tunajaribu pia kuunga mkono wito wa Rais Kikwete wa kuimarisha zaidi uwazi, pamoja na kupiga vita rushwa.
Njia moja tunayotumia kufanikisha masuala haya ni kupitia sheria ya taasisi ya Millennium Challenge. Hii ina mpango wa awali unaoitwa Threshold Program, ambao lengo lake ni kuimarisha asasi za kiraia, pamoja na waandishi wa habari katika kazi yao kama ‘walinzi’ dhidi ya rushwa.
Idadi ya habari zinazoandikwa kila mwezi kuhusu rushwa nchini Tanzania imeongezeka mara saba. Tunaamini mpango huo wa wa awali umesaidia kuhamasisha hilo.
Mpango huo pia unafadhili mifumo ya kufuatilia matumizi ya umma (PETS -- Public Expenditure Tracking Systems), ambayo imeanzishwa nchini kote Tanzania, ikiwa ni pamoja na hapa Zanzibar.
Nimepata fursa ya kutembelea sehemu nyingi zinazotekeleza mfumo wa PETS katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Morogoro. Lilikuwa ni jambo zuri sana kuona wananchi wa kawaida wakija pamoja kuhamasisha uwazi. Ilikuwa inasisimua kuwaona Watanzania hawa wema wakipata taarifa zaidi kuhusu fedha za umma, na jinsi zinavyotumika.
Miradi hii ya PETS ni ishara kuwa demokrasia itapata nguvu zaidi katika miezi na miaka ijayo. Pia ni ishara kuwa, wananchi wanataka kutokomeza aina zote za rushwa. Rushwa ni kosa la jinai dhidi ya wananchi wa Tanzania.
Mpango huo wa awali, yaani Threshold Program, unatangulia mkataba wa msaada kutoka kwenye mfuko wa Millennium Challenge Account. Ninafurahi kutangaza kuwa jana, mjini Washington D.C., bodi ya wakurugenzi ya taasisi ya Millennium Challenge Corporation (MCC) ilikutana na kuunga mkono rasmi mkataba wa msaada huo kwa Tanzania, huu ukiwa ni msaada mkubwa zaidi kuliko yote katika historia ya mpango huo.
Hatimaye utakapotiwa saini mapema mwaka kesho, msaada huo utatoa dola milioni 698 kwa kipindi cha miaka mitano, kusaidia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, nishati, pamoja na maji safi nchini kote.
Zanzibar ni sehemu muhimu ya msaada wa MCC. Takriban kilometa 35 za barabara vijijini zitajengwa kisiwani Pemba. Mafungu ya fedha yatatolewa pia kuhakikisha barabara zinakarabatiwa mara kwa mara, ili kuongeza uwezo wa Tanzania kutunza mtandao wa barabara zake.
Mradi wa kuunganisha umeme wa Zanzibar unahusisha kuwekwa kwa waya mpya wenye urefu wa kilomita 40 na nguvu ya megawati 100 chini ya bahari, utakaoleta nishati ya kuaminika hapa visiwani. Hii itaiwezesha Zanzibar kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa kisiwa hiki. Lakini, kuna kitu kinachofanya msaada wa MCC kuwa tofauti na mipango mingine, na nchi zingine. Msaada huu si ruzuku. Bali ni mkataba kati ya Marekani na Tanzania. Utakapotiwa saini, msaada huu utaziwekea nchi zetu mbili wajibu mpya.
Hapa Tanzania, serikali inaahidi kuweka msisitizo mpya kwenye uwazi na vita dhidi ya rushwa. Serikali pia inaahidi kuleta mageuzi, pamoja na kuweka nyenzo za kupima mageuzi hayo.
Kwa maneno mengine, kutia saini kwa mkataba wa msaada huo siyo mwisho wa jambo, bali ni mwanzo wa ukurasa mpya katika utawala bora, pamoja na urafiki mpya baina ya nchi zetu na wananchi wetu. Kwangu mimi, hili ni jambo la kusisimua sana.
Ni muhimu kwamba tuko hapa kuongelea mambo haya. Nyumba hii ni ishara ya sehemu ya historia kati ya mataifa yetu. Leo, nyumba hii ni ishara ya sehemu ya mustakabali wetu!
Tunafurahia mustakabali huo. Hebu niwahakikishie, kama Balozi, kwamba Marekani itatoa msaada wetu, pamoja na kusimama bega kwa bega na wananchi wa Zanzibar, kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma, kwa zaidi ya miaka mia mbili.
Asanteni sana!



